MAAFISA USAFIRISHAJI GINERY WARUDISHA KWA JAMII HOSPITALI YA MANDEWA

Na Saulo Stephen – Singida.

Katika kurejesha kwa jamii, Maafisa Usafirishaji wa kijiwe namba 7 mtaa Ginery Mkoani Singida, wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwenye wodi ya akina mama na watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida Mandewa.

Akiongea wakati wa kukabidhi mahitaji hayo katika wodi hiyo katibu wa kijiwe cha maafisa Usafirishaji Ginery, Miraji Ntunda amesema lengo la kutoa msaada huo ni kuhakikisha wanaigusa jamiii kwa namna mungu alivyowajalia huku akiwaasa makundi mengine pamoja na watu wenye uwezo kujenga utamaduni wa kutoa misaada mbalimbali kwa watu wenye mahitaji ili kuonyesha upendo na kuwapa faraja watu wenye mahitaji.

Vitu vilivyotolewa na maafisha usafirishaji hao ni pamoja na sabuni ya unga,sabuni ya kipande,pamoja na maziwa ya unga kwa ajili ya watoto pamoja na akina mama wanaonyesha waliolazwa katika Hospitali hiyo.

Kwa upande wake Muuguzi kutoka Wodi ya kina mama na Watoto Dkt. Rukia Ibrahim akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa amewashukuru maafisa usafirishaji wa kijiwe namba 7 Ginery kwa kutoa msaada huo huku akiwaomba kuendelea kutoa msaada kwa makundi mengi kwa kadri watakavyojiliwa na mwenyezi Mungu, kwani kwa kufanya hivyo ni sehemu ya sadaka.

Nao baadhi ya maafisa usafirishaji waliofika katika zoezi hilo wameiambia jambo fm kuwa wameamua kufanya jambo hilo sio kwa sababu ni matajiri ,bali ni moyo tu ambao umewasukuma kuchangishana kwa umoja wao na kuamua kugusa mahitaji ya watu wenye mahitaji wakiwemo akina mama na watoto wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida Mandewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *