MAAFISA KILIMO SHINYANGA WAJENGEWA UWEZO USALAMA WA CHAKULA, UFUATILIAJI MAZAO

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Maafisa Kilimo kutoka Halmashauri  zote sita za Mkoa wa Shinyanga wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kutambua na kutumia mbinu bora za ukusanyaji wa taarifa kuhusu hali ya mazao shambani na usalama wa chakula kwa mtumiaji.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Kilimo Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo,  Robert Dimojo, amesema Serikali kupitia Wizara ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini kwa kufanya tathmini ya uzalishaji, upatikanaji na hali ya lishe kwa ujumla.

Amesema  kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wataalamu hao kutumia mbinu na nyenzo za kisasa katika ukusanyaji wa taarifa sahihi na za kuaminika, zitakazosaidia kupanga mikakati madhubuti ya kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Aidha, Maafisa Kilimo kutoka halmashauri mbalimbali walipata fursa ya kuwasilisha hali ya mazao katika maeneo yao, wakieleza ukuaji wa mazao, changamoto za visumbufu vya mazao pamoja na mwenendo wa mvua, sambamba na mbinu wanazotumia kukusanya taarifa hizo.

Usalama wa chakula ni hali ya kuhakikisha kuwa chakula kinachotumiwa na watu ni salama, safi, na hakina madhara kwa afya. Hii inahusisha hatua zote kuanzia uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi hadi upishi wa chakula.

Kwa mtumiaji, usalama wa chakula ni muhimu ili kuepuka magonjwa yanayosababishwa na bakteria, virusi, au kemikali hatari. Mtumiaji anapaswa kuhakikisha kuwa chakula kinapikwa vizuri, kinaoshwa kabla ya kuliwa (hasa matunda na mboga), na kinahifadhiwa katika mazingira safi na yenye joto linalofaa.

Pia ni muhimu kuangalia tarehe ya mwisho wa matumizi wa bidhaa, kuepuka kula chakula kilichoharibika, na kudumisha usafi wa mikono kabla ya kushika au kula chakula. Kwa kufanya hivyo, mtumiaji anaweza kulinda afya yake na ya familia kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *