MAADHIMISHO YA MIAKA 63 YA UHURU MKOANI SHINYANGA

NA EUNICE KANUMBA -SALAWE

Maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara yamefana katika mkoa  wa Shinyanga ,huku Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,akimuakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha  akielezea mafanikio katika sekta mbalimbali  ambayo yamepatikana    mara baada ya nchi taifa  kupata uhuru mwaka 1961.

Amesema baada ya nchi kupata uhuru, hadi sasa imepiga hatua kubwa kimaendeleo,huku pato la mwananchi katika Mkoa wa Shinyanga, likiongezeka na kufikia milioni 1.9 kwa mwaka.

Aidha, Dc Mtatiro amesema mwaka 1961 katika sekta ya kilimo asilimia 75 ya wakulima walikuwa wakitumia zana duni, na hivyo kufanya kuwepo na uvunaji mdogo wa mavuno,lakini sasa hivi Tenknolojia imekua, na wakulima wamekuwa wakilima kisasa na kupata mavuno mengi.

Amesema mwaka 1961 Mkoa wa Shinyanga haukuwa na Viwanda Vikubwa na Kati, lakini baada ya kupata uhuru ,hadi sasa kuna Viwanda Vikubwa 40, huku viwanda vya kati vikiwa Kati 192, na viwanda Vidogo  mpaka sasa ni 1,225.

Amesema kwa upande wa umeme hadi sasa vijiji 485 vina huduma ya nishati hiyo na katika elimu jumla ya ,shule za awali na msingi 635 zimejengwa ambazo hazikuwepo, huku madarasa 1,663 yakijengwa pamoja na shule 15 za wanafunzi zenye ulemavu.

“Miaka hiyo hapa Shinyanga kulikuwa na shule moja tu ya Sekondari ambayo ni Shybush, lakini sasa hivi zipo shule 190 na nyingine 8 zinajengwa,”amesema Mtatiro.

Amesema katika sekta ya maji kulikuwa na visima 16,lakini sasa wananchi wa mjini wanapata maji asilimia 73 na vijijini asilimia 68,huku huduma za afya zikiongezeka,pamoja na upatikanaji wa majosho ya kuoshea mifugo 91 na marambo 54.

Katika hatua nyingine,amewataka wananchi kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa kipindupindu,huku akiwasisitiza pia kupanda miti pamoja na kufanya kilimo chenye tija.

Mtatiro pia amewasihi wananchi kupima afya zao mara kwa mara,pamoja na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) ili kujua afya zao.

Nao baadhi ya wazee  waliokuwepo wakati taifa la Tanganyika likipata uhuru  mwaka 1961 akiwamo Benard Itendele na Spora Pangani,wamesema kabla ya nchi kupata uhuru watu walikuwa akiishi kama wanyama chini ya wakoloni,lakini sasa hivi maisha ni mazuri na huduma zote za kijamii zinapatikana.

Katika maadhimisho hayo yalitanguliwa pia na zoezi la upandaji miti,upimaji wa virusi vya ukimwi,ushauri nasaha, pamoja na mpira wa miguu.

Maadhimisho hayo , kimkoa yamefanyika katika kijiji cha Songambela kilichopo katika  Kata ya Salawe halmashuri ya wilaya Shinyanga yakichagizwa na michezo mbalimbali ikiwemo soka ngoma za asili pamoja mdahalo uliochagizwa na wazee waliokuwepo  wakati Tanganyika ikipata uhuru wake toka katika nchi ya Uingereza.

 Kauli mbiu katika maadhimisho mwaka huu ni “Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wananchi ni msingi wa maendeleo”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *