Na Saada Almasi – Simiyu.
Wakulima wa nyanya katika kata ya Lamadi na Kabita Wilayani Busega mkoani Simiyu wanaojihusisha na kilimo hicho kandokando ya ziwa Victoria wameiomba serikali kushirikiana nao katika kusimamia zuio la usafirishaji wa matenga yanayozidi viwango yaani lumbesa ambayo kwa kiasi kikubwa yanaua mitaji yao.
Akizungumza na Jambo Fm Salome John mkulima kata ya Kabita amesema kuwa licha ya kuazimia idadi ya debe tatu tu kupimwa katika tenga moja wanunuzi huwagalaliza kiasi cha kuchukua debe tano kwa tenga hali inayosababisha kushindwa kulipa madeni ya mikopo ambayo huichukua kama mitaji ya kufanyia shughuli hizo na kuwafanya kuurudia umasikini.
Amesema, “tunachukua pesa za mama Samia ambazo zinakopeshwa ili kutusaidia wananchi tujikwamue lakini jinsi ya kurejesha inakuwa ngumu tunalima sawa lakini mauzo hatuyaoni mwisho tunaurudia umasikini.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakulima wa Nyanya Busega, Bujiku Mathias amewataka wakulima wa zao hilo kuungana kupinga lumbesa sambamba na kuitaka serikali kuzidisha ukaguzi katika vituo vya ukaguzi vya Lamadi na Mara ambavyo inasemekana wanunuzi wa zao hilo hupenyeza matenga yao katika magari na kukwepa ukaguzi.
“Haya matenga yanapita kwenye vituo vya ukaguzi kinyemela sana geti la Lamadi na Mara tunaomba serikali iwe makini wawakamate hawa walanguzi ili tukomeshe tabia hii lakini pia niwatake wakulima wote tuungane tuipinge lumbesa kwani ni kwa faida yetu sote,” alisema Bujiku.
Licha ya malalamiko hayo bado wanunuzi wamekuwa wakivutia kamba upande wao kwa kusema kuwa ukubwa wa tenga haumfanyi mkulima kupima zaidi ya debe tatu kwani wao hununua sehemu yoyote ikiwa ni pamoja na Igoma jijini Mwanza ambapo vipimo ni tofauti hivyo huheshimu kipimo cha mkulima.

Akisisitiza, mnunuzi na mfanyabiashara wa zao hilo Kata ya Lamadi, Rebeca Merengo amesema, “sisi hatuangalii wapi kwa kununua tunaangalia upatikanaji wa mzigo watuambie ni kipimo gani tunatakiwa kufuata ili mimi hata nikija na tenga kubwa kipimo chako ndicho kitumike maana tukienda kununulia mwanza tunaheshimu vipimo vyao.”
Kwa kawaida tenga moja linalokuwa na debe tano za nyanya huuzwa kwa shilingi elfu 25 wakati kipimo stahiki ni kile cha debe tatu za nyanya kwa kila tenga hivyo mkulima anapoteza debe mbili za nyanya kila anapouza tenga moja.
Hata hivyo, Ngimba Soja ambaye ni mmoja wa wakulima hao ametoa wito kwa serikali kuwajengea kiwanda cha zao hilo ili kupunguza upotevu wa nyanya ambao ungetumika na kuwapa faida ili mikopo wanayochukua ilipike kirahisi.

“Maeneo haya hatuna kiwanda cha nyanya niiombe serikali watujengee kiwanda ili haya mazao yetu tuyapeleke pale ambapo kutakuwa na biashara ya uhakika tunagharamika sana kununua madawa na mbolea lakini tukiwa na sehemu moja ya kuuza tutaweza hata kulipa mikopo yetu,” alisema Ngimba.
Desemba 30, 2024 wakulima wa maeneo hayo walitoa malalamiko kwa serikali na kuitaka kuweka zuio la lumbesa na hadi kufikia Januari 7 2025 zuio hilo lilipitishwa japokuwa bado baadhi ya walanguzi wanaendelea kuwaumiza wakulima.