Na Saada Almasi -SIMIYU
Viongozi ,wazazi na walezi wa Watoto mkoani Simiyu wametakiwa kulinda haki za Watoto hususan wanafunzi na kuwakinga dhidi ya vitendo vya kikatili na unyanyasaji wa kijinsia ili waishi kwa amani na kufanikiwa kutimiza ndoto zao.
Wito huo umetolewa na mkuu wa mkoa huo Kenani Laban Kihongosi alipokuwa akifungua wiki ya sheria mkoani humo ambapo amesisitiza utayari wa kila mmoja katika kuwalinda Watoto wa kike ambao mara nyingi huingizwa katika ndoa za utotoni.
“Niwaombe wadau wa elimu na wananchi kwa ujumla mtoe taarifa kwa mamlaka husika pale mnapoona viashiria vya ukatili wa kijinsia ili sheria isimamie na haki iweze kupatikana ili kusiwe na mwanafunzi aliyeshindwa kumaliza shule kwa kuolewa au kubeba mimba” – Kihongosi.
Inaelezwa kuwa mfumo wa Maisha ulioathiriwa na mila na desturi za mkoa huu za kutothamini mchango wa elimu kwa mtoto wa kike ndiyo haswa umekuwa chanzo cha kukatisha ndoto za Watoto wa kike.Makabila mengi ya mkoa huu hawsa wanyantuzu na wasukuma kwao mtoto wa kike anapojitambua huhesabika kama faida ya kuleta ng’ombe nyumbani kama ambavyo ameeleza Moses Mashimba mkazi wa mkoa huu.
“Huu ukatili unaanzia nyumbani kwa sababu mtu anamuona mwanae wa kike kama mali anaamini mtoto akikua anatakiwa kuozeshwa ili alete ng’ombe nyumbani hii ni desturi tuliyokua nayo kwa hivyo mabadiliko yanatakiwa kuanzia nyumbani nadhani wapewe elimu ” – Moses.
Kwa upande wake Gwanu Mlamo ambaye ni msichana na mwanafunzi wa kidato cha tatu mkoani humo ameiomba serikali kutilia mkazo sheria na adhabu mbalimbali ambazo atakumbana nazo mzazi yeyote ambaye anashiriki kukatiza ndoto za mtoto wa kike kwa lengo la kujinufaisha.
“serikali iongeze sheria na ziwe wazi kwa kila mtu ili pale anapokuwa na mawazo ya kufanya ukatili kwa kukatisha ndoto zetu ajue kabisa atakabiliana na adhabu gani hiyo itatusaidia kutimiza ndoto zetu” – Gwalu.
Ufunguzi wa wiki ya sheria mkoani hapa imehusisha baadhi ya tasisi za kisheria kuweka kambi kwa wiki moja huku wakitoa elimu na msaada wa kisheria sambamba na kupokea maoni ya wananchi juu ya masuala mbali mbali ya kisheria.