
NA EUNICE KANUMBA –KISHAPU,SHINYANGA
SERIKALI wilayani Kishapu imezindua rasimi zoezi la utoaji wa chanjo ya mifugo pamoja na uwekaji wa hereni kwa wanyama lengo likiwa ni kukabiliana na mlipuko wa magonjwa kama vile homa ya mapafu kwa ng’ombe na punda na ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo pamoja na ugonjwa kideri kwa mifugo jamii ya ndege, pamoja na kufanya utambuzi wa mifugo wilayani humo.
Zoezi hilo limezinduliwa leo tarehe 16 september 2025 katika kata ya Mwamashele, na mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi, kwenye mbuga ya kufugia wanyama ya mwekezaji katika sekta ya ufugaji na kilimo Ardi Hillal Hamad ambapo jumla ya mbuzi na kondoo 251 wamechanjwa pamoja na ng’ombe 269.
Aidha DC Masindi ametumia jukwaa hilo kuwataka wafugaji kuleta kwa wingi mifugo yao ipatiwe chanjo ili iweze kustawi kwa kukingwa na magonjwa nakuwasihi fedha zitokanazo na mauzo ya mifugo hiyo zihudumie familia kwa kununua mahitaji pamoja na kusomesha watoto wa jinsia zote katika familia husika.
“Niwaombe wafugaji mjitokeze kwa wingi kuleta mifugo yenu ipatiwe chanjo ili kuweza kukabiliana na mlipuko wa magonjwa na hatimae mfuge kwa ustawi” amesema Masindi.

Naye mratibu wa chanjo za mifugo wilayani Kishapu John Mchele ameelezea umuhimu wa uwekaji hereni kwa mifugo kuwa ni pamoja na kufahamu idadi ya wafugaji katika kuwahudumia katika masuala mbalimbali yakiwemo malisho na kuanisha kuwa serikali imetoa dozi laki nne na nusu kwa ajili ya chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe lakini pi imetoa dozi laki nne na elfu arobaini na mbili kwa ajili ya ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo.

Aidha Mchele ameanisha kuwa serikali imetoa pia dozi laki tatu ili kukabiliana na ugonjwa wa mafua ya mifugo jamii ya ndege.
Mchele amesema lengo ni kuwafikia wafugaji wote katika kata zote ishirini na tisa za wilaya hiyo na katika vijiji vyote 117 nakuaanisha kuwa lengo la serikali kwa sasa ni kuona sekta ya mifugo inaimarika.
Kwa upande wake afisa kilimo na mifugo Mwita Mwijarubi amesema serikali inadhamira njema hivyo amewataka k wananchi kuleta mifugo ipatiwe chanjo kwani itaepukana na magonjwa na kuongezeka thamani na kupata nafasi ya kuiuza hata nje ya nchi.
Nao baadhi ya wafugaji waliojitokeza katika kambi hiyo akiwemo Daud Gamaya amesema chanjo hiyo wameipokea kwa shangwe kwani wamekuwa wakihangaika na magonjwa kwa ng’ombe ,mbuzi na kondoo pamoja na kuku, kwani mifugo ilikuwa inakufa sana kwa sasa mifugo yao itakuwa salama.
Lakini pia Chagu Maige mfugaji kutoka katika kijiji cha Mwamashele ameishukuru serikali kwa kuweka ruzuku katika chanjo za mifugo kwani hapo awali walikuwa wanahangaika sana kwa matatizo ya magonjwa ya mifugo lakini sasa mifugo yao imechanjwa shida ya mifugo kufa kwa magonjwa inakwenda kuisha.


