
Wamiliki wa shule wenye magari yanayobeba wanafunzi katika mkoa wa Mwanza wametakiwa kuyakagua na kuyafanyia matengenezo magari yao kabla ya kufunguliwa kwa muhula mpya wa masomo unaotarajia kuanza mapema Januari 2025.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Aloyce Nyantora kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza wakati akizungumza na wamiliki wa shule, wasimamizi wa sheria, Madereva na wadau wa usafirishaji mkoa wa Mwanza ambapo amesema kwa sasa zoezi la kuyakagua magari hayo ni la hiari na kwa wale wote watakaokaidi kupeleka magari hayo kwenye ukaguzi kabla ya shule hazijafunguliwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Katika hatua nyingine ACP Nyantora pia amewataka wamiliki wa magari hayo kuzingatia idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kukaa kwenye magari yao kwani wapo baadhi yao ambao wamekua wakijaza watoto wa shule zaidi ya uwezo wa gari jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza Mrakibu wa Polisi (SP) Sunday Ibrahim amesema kikosi cha usalama barabarani kimejipanga kikamilifu katika kusimamia zoezi hilo la ukaguzi ambalo limepangwa kufanyika kwenye vituo vya Polisi vya wilaya ambapo kwa wilaya ya Nyamagana na Ilemela zoezi litafanyika katika kituo cha mabasi Nyamhongolo.
Nae, Afisa Elimu mkoa wa Mwanza Martine Nkwabi amewaasa wamiliki wa shule kuacha kutumia magari mabovu kubeba wanafunzi,huku pia akiwataka wamiliki ambao magari yao yana vioo vya giza ( tinted) kuviondoa vioo hivyo kwani havikubaliki kwenye magari ya wanafunzi.
Aidha pia amewataka wamiliki wa shule kuhakikisha kila gari la kubebea wanafunzi linakua na muhudumu wa kike( matron) ili kupunguza vitendo vya ukatili ambavyo vimekua vikitokea kwenye magari ya wanafunzi.
Kwa siku ya leo zaidi ya magari 50 yamekaguliwa ambapo magari 37 yamekutwa ni mazima na magari 15 yamekutwa na hitilafu na wamiliki wake wametakiwa kuyatengeneza kabla ya kuyaingiza barabarani.


