LAAC YAANZA KUWAHOJI VIONGOZI WA HALMASHAURI 39 KUHUSU HOJA ZA CAG

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeanza kuwahoji viongozi wa Halmashauri 39 kutoka mikoa 15 nchini kuhusu hoja zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo Agosti 4,2026 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ado Shaibu amesema zoezi hilo linafanyika kwa niaba ya Bunge baada ya kupata kibali cha Spika wa Bunge, ambapo katika hatua ya awali kamati ilihoji halmashauri Nane wakati wa Bunge la Bajeti, huku hatua ya sasa ikihusisha halmashauri 39.

Kwa mujibu wa Kamati, viongozi wa halmashauri, hususani wakurugenzi na timu zao za menejimenti, wanatakiwa kutoa maelezo kuhusu hoja zilizobainishwa na CAG pamoja na kueleza hatua walizochukua kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa awali.

Mbali na kuchambua hoja hizo, Kamati pia inafuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Bunge na mapendekezo ya CAG yaliyolenga kuondoa dosari katika matumizi ya fedha za umma.

Ado ameeleza kuwa jukumu la LAAC ni kubaini sababu za matumizi yasiyo sahihi ya fedha za serikali za mitaa, kusikiliza utetezi wa wahusika na kutoa mapendekezo ambayo baadaye yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya maamuzi na maazimio ya Serikali.

Zoezi hilo lilianza kwa halmashauri za Mkoa wa Singida na linaendelea katika mikoa mbalimbali ikiwemo Kigoma, Tabora, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Shinyanga, Geita, Mara, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.

Pia Kamati imesisitiza kuwa lengo la zoezi hilo si kuwabana viongozi wa halmashauri pekee, bali kuhakikisha fedha za wananchi zinatumika kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia sheria, ili kuongeza thamani ya miradi na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Zoezi hilo linatarajiwa kutoa taswira ya namna halmashauri zinavyotekeleza wajibu wao wa usimamizi wa fedha za umma, huku likitoa fursa ya kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kwa maslahi ya wananchi na maendeleo ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *