KUWASA WATAKIWA KUHARAKISHA ZOEZI LA KUBAINI, KUONDOA MIUNDOMBINU YA ZAMANI

Watumishi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji  KUWASA wametakiwa kuharakisha zoezi la kubaini, kuondoa na kudhibiti miundombinu ya zamani inayopitisha maji katika maeneo mbalimbali ya wananchi.

Hayo yamelezwa na Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka hiyo Dkt. Christopher Nditi wakati wa kikao maalum na Idara ya Ufundi na Uzalishaji Maji kilicholenga kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya maji katika eneo la Bwawa la Katubuka.

Katika kikao hicho, Dkt. Nditi ametoa maelekezo ya kuharakishwa kwa zoezi la kubaini, kuondoa na kudhibiti miundombinu ya zamani inayopitisha maji katika eneo hilo, ambalo hapo awali lilikuwa makazi ya wananchi kabla ya kufunikwa na maji.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza upotevu wa maji unaoweza kusababishwa na uvujaji wa miundombinu iliyobaki chini ya maji. Kwa mujibu wake, hali hiyo inaweza kuwa moja ya sababu zinazochangia eneo hilo kuendelea kuwa na maji kwa muda mrefu tangu lilipojaa mwaka 2022.

“Tunapaswa kuchukua hatua za haraka kulinda rasilimali ya maji kwa kuhakikisha miundombinu yote inayoweza kusababisha upotevu wa maji inadhibitiwa kwa wakati,” amesisitiza Dkt. Nditi.

Mbali na hilo, Dkt. Nditi amewataka mafundi na wataalamu wa KUWASA kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kushughulikia changamoto za kiufundi. Amesema masuala yanayohusu miundombinu ya maji yanahitaji kujadiliwa na kutatuliwa kwa pamoja na wataalamu mbalimbali ili kupata suluhisho la haraka, sahihi na lenye manufaa kwa wananchi.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya utekelezaji, Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji, Mhandisi Francisco Makoye, amesema kazi imeanza rasmi na tayari timu ya wataalamu imefanikiwa kubaini baadhi ya mabomba makubwa yaliyobaki katika eneo la Bwawa la Katubuka.

Makoye amebainisha kuwa zoezi la kudhibiti miundombinu hiyo linaendelea vizuri na linatarajiwa kukamilika ndani ya muda mfupi, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi wa usimamizi wa maji na kupunguza upotevu wa rasilimali hiyo muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *