Na Saulo Stephen – Singida.
Mwenyekiti wa bajaji mkoa wa Singida, Abdul Swalehe Mitigo, amesema kuwa licha ya kupanda kwa bei ya mafuta, bado hakuna kiwango maalum kilichowekwa cha nauli kwa vyombo hivyo.
Akizungumza na Jambo Media, Mitigo ameeleza kuwa bajaji ni chombo cha kukodi, hivyo gharama ya nauli hutegemea makubaliano kati ya dereva au mmiliki wa bajaji na mteja husika.

Amefafanua kuwa tofauti na daladala au mabasi yenye nauli zilizopangwa, bajaji hutoa huduma ya kubeba abiria kulingana na mazungumzo ya pande mbili, hali inayoweza kusababisha utofauti wa bei kutoka eneo moja hadi jingine.
Hata hivyo, amewasihi madereva wa bajaji kuzingatia utu, uadilifu na hali halisi ya maisha ya wananchi wakati wa kupanga nauli, ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wateja.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunapaswa kuzingatiwa, lakini pia wameomba kuwepo kwa uwazi na uelewa mzuri ili kuepusha kutozwa nauli kubwa kupita kiasi.
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) mkoa wa Singida Anord Selwada amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna mabadiliko rasmi ya nauli yaliyotangazwa kwa vyombo vya usafiri vinavyodhibitiwa.


