Waziri wa Elimu wa Ufaransa Gabriel Attal ametangaza kuwa Nchi hiyo imelazimika kufunga Shule saba zinazowapokea Wanafunzi 1,500 baada ya kuvamiwa na kunguni.
Mapema wiki hii, Mamlaka ya Paris ilitangaza kufungwa kwa Shule mbili kwa sababu ya kunguni, moja huko Marseille na nyingine Villefranche-sur-Saone nje kidogo ya Mji wa kusini mashariki wa Lyon.
Serikali ya Ufaransa imefanya mfululizo wa mikutano wiki hii kuchunguza idadi inayoongezeka ya matukio ya kunguni, wakati Nchi hiyo ikiandaa Kombe la Dunia la Rugby na ambayo itakuwa Mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki hapo mwakani.
Serikali mjini Paris imelazimika sasa kuingilia kati kupambana na kunguni hao ambapo Waziri Mkuu wa Ufaransa Elisabeth Borne ameitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kujadili namna ya kupambana na kunguni.
Waziri wa Usafiri Clement Beaune pia amekutana na makampuni ya usafirishaji kubuni mpango wa kufuatilia na kunyunyizia dawa vyombo vya usafiri wa umma na kujaribu kupunguza wasiwasi.