Wanawake wenye maono na kutamani kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wametakiwa kutokata taamaa na kutosikiliza maneno ya watu wanaowakatisha tamaa wengine.
Kauli hiyo, imetolewa na Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Christina Mnzava na kuongeza kuwa Mwanamke anatakiwa ajiamaini na kujikubali kuwa anaweza.
Amesema, “nilianza kuwa kiongozi tangu nasoma na hata nilipoingia kazini pia niliendelea kuwa kiongozi na niliingia katika siasa tangu mwaka 1988 na ilipofika mwaka 2002 nikagombea siasa ngazi ya Wilaya Shinyanga vijijini nikapata nafasi zote mpaka kuingia kamati ya maadili na mkutano mkuu Taifa yote haya niliyafanya nikiamini ninachokisimamia.”

Dkt. Mnzava ameongeza kuwa, kupata nafasi hizo za uongozi zilimpa hamasa zaidi ya kujiona kuwa ni kiongozi nakutamani kuongoza kundi la wanawake na kuanzia hapo akajipa ujasiri wa kuijtosa kwa nafasi ya Ubunge.
Aidha, amesema mwaka 2010 aligombea nafasi ya Ubunge ambayo ilikuwa na ushindani uliojumuisha wanawake wenye majina makubwa na waliokuwa na watu nyuma yao lakini hali hiyo haikumkatisha tamaa ya kuwa kiongozi.
Hata hivyo, amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kiliendelea kumuamini kutokana na utendaji kazi wake kama kiongozi na mwaka 2014 aliteuliwa kuwa Mbunge katika Bunge la Katiba na kuwakilisha kundi la Wachimbaji.

“Mwaka 2010 niligombea na watu magiant sikuogopa nikapambana nikashindwa nilikuwa mtu wa tatu mwaka, 2015 nikaingia tena nikawa mtu wanne lakini sikukata tamaa licha ya kukatishwa tamaa na ndugu na watu wangu wa karibu mwaka 2020 nikiwa nafanya kazi nje ya nje bila kushirikisha ndugu zangu niligombea na tena bila kutoa fedha yeyote kwa wanawake na nikapata,” alisema Dkt. Mnzava
Ameongeza kuwa, matamanio yake ya kuwa kiongozi yalianza tangu akiwa mtoto na kilichomshawishi kuingia katika siasa na kuwa kiongozi ni kusoma vitabu na kufuatilia kwa karibu maisha ya wanawake viongozi waliofanikiwa na hao walimpa hamasa ya kufikia matarajio yake.
Ameitaja siri ya mafanikio ya nafasi zake za uongozi kuwa ni kupenda kazi anayoifanya, kujiamiani na mashiriakiano na wanawake na kwamba anaamini kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake amewatendea haki wanawake wa Shinyanga kwa nafasi ya Ubunge na kuahidi kuitetea katika uchaguzi ujao.
Mnzava pia ametoa wito kwa wanawake wote katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotaraijwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu kusimamia malengo yao na kutotegemea mawazo ya mtu hasa walio kwa ajili ya kukatisha tamaa wengine.