
Mkuu wa wilaya ya Handeni, Wakili Alberto Msando amewataka Wasafiri wote wanaopita wilaya ya Handeni kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama wa barabarani na ametoa onyo kwa yoyote anayempigia simu baada ya kukamatwa na askari waache mara moja.
Msando ameyasema hayo kwenye post yake kwenye mtandao wa Kijamii wa Instagram baada ya kupost picha za ajali iliyotokea leo (Desemba 24) majira ya saa 12 ya asubuhi.
Msando ameandika ‘Leo asubuhi mida ya saa 12 imetokea ajali iliyohusisha Lori na Coaster. Ajali hiyo imetokea eneo la Michungwani, Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni. Watu 7 wamepoteza maisha na 10 wamejeruhiwa.’ – DC Msando.
Naendelea kuwasisitiza sana madereva kuwa makini na kuchukua tahadhari. Ajali hii sababu ni UZEMBE WA DEREVA. Kwa sababu ya kujirudia rudia kwa UZEMBE nimemuelekeza OCD atakayekiuka sheria ya barabarani eneo la Handeni tutampandisha Mahakamani na kuomba adhabu ya kifungo. -DC Msando.
Kwa ambao mmekuwa mkipiga simu kusaidiwa madereva wenu wakikiuka sheria za barabarani wala msisumbuke: HAKUNA MSAADA ZAIDI YA KUKAA LOCK UP KWA MUJIBU WA SHERIA NA KUPANDISHWA KIZIMBANI. – DC Msando.
Ukifika kijiji cha Manga Wilaya ya Handeni ewe Dereva usipofuata sheria za usalama barabarani USITULAUMU. Ajali nyingi zinaepukika. Na abiria, acheni kukaa kimya wakati dereva anaendesha hovyo aidha SHUKA utarejeshewa nauli yako na toa taarifa kwa Jeshi la Polisi tudhibiti huu uzembe. TUSHIRIKIANE 🙏🏿🙏🏿’. – DC Msando.



