KUFUATIA AJALI ZA BARABARANI, RAIS SAMIA ATOA MAELEKEZO HAYA..

Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama kuongeza umakini kwenye usimamizi wa sheria za usalama barabarani.

Rais Samia ameyasema hayo wakati anatoa pole za Watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya Coaster na Lori la mizigo eneo la Mikese Morogoro.

Rais Samia ameandika Madereva ‘Usiku wa kuamkia leo Desemba 18 2024 tumepoteza ndugu zetu 15 kwa ajali ya barabarani, iliyohusisha lori la mizigo na gari la abiria aina Coaster katika eneo la Mikese, Barabara Kuu ya Morogoro – Dar es Salaam (A7 Highway)’. – Rais Samia

‘Ninawapa pole familia, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Adam Malima, ndugu, jamaa na marafiki. Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu ndugu zetu hawa wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka’. – Rais Samia.

‘Mbali na wito wangu kwa umma na maelekezo niliyolipa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama Desemba 4 mwaka huu kuhusu kuongeza umakini na usimamizi katika Sheria za Usalama Barabarani, leo nimeliagiza Jeshi la Polisi kuwa na mfumo wa Leseni za Udereva utakaoweza kuwapunguzia alama (points) madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama na uhai barabarani’. – Rais Samia.

‘Mfumo huu uweke taarifa (records) kielektroniki za mwenendo wa makosa ya madereva barabarani kitakwimu, na kisha tumike kuamua kama wanastahili kuendelea kuwa na leseni za udereva au la. Hii ni katika kuboresha mfumo wa sasa ambao mara nyingi dereva hulipa faini pekee na kuachwa kuendelea kuwepo barabarani.’ – Rais Samia.

‘Uhai wa binadamu hauna mbadala, na hatuna budi kuendelea kuchukua hatua za pamoja na madhubuti kuhakikisha unalindwa kwa nguvu zote. Hatua hizi ni pamoja na kuhakikisha vyombo vya moto vinavyoingia barabarani vina sifa na vigezo vya kutumia barabara, na wale wanaoviendesha wana sifa, vigezo na rekodi za kustahili kuendelea kufanya hivyo’. – Rais Samia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *