Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, limeuarifu umma kuwa kifo cha Askari namba. H.1796 Koplo Mwita, aliyekuwa akishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi katika kituo cha Polisi Wilaya ya Tanga kimetikana na kukosa hewa baada ya kujinyonga.
Taarifa iliyotolewa hii leo Agosti 31, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga imeeleza kuwa, Askari huyo alikutwa akiwa amefariki Dunia ndani ya chumba cha mahabusu katika kituo hicho Agosti 27, 2026 majira ya saa moja na dakika tatu usiku.

Inaarifiwa kuwa kabla ya kifo chake, marehemu, Afisa mmoja na Askari watano wa Jeshi la Polisi wa vyeo mbalimbali, walikuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kijinai.
Kufuatia kifo cha askari huyo, uchunguzi wa kisayansi uliofanyika na ndugu zake kushuhudia ulibaini chanzo cha kifo chake ni kukosa hewa kutokana na kujinyonga ambapo mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.



