
Na Saada Almasi-Bariadi,Simiyu
Watanzania wametakiwa kujitoa na kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu kwa njia ya amani na utulivu na kujiweka mbali na mikwaruzano itakayopelekea machafuko ambayo mara zote husababishwa na wachache wasio na uchungu wa nchi yao.
Rai hiyo imetolewa na katibu tawala halmashauri ya wilaya ya Bariadi Justine Manko katika kongamano la watuma salamu kitaifa ambali limefanyika mjini Bariadi mkoani Simiyu na kuhusisha uchaguzi wa viongozi wa watuma salamu Tanzania ambapo amewataka wajiepushe na makandokando yoyote yanayoweza kuiweka nchi katika hatari.

“Leo hii mpo katika uchaguzi ni imani yangu mtafanikisha kwa amani na upendo vivyo hivyo niwatake kujiepusha na lolote litakaloiweka nchi rehani kipindi cha uchaguzi mkuu,najua mna nguvu kubwa tuitumie kuhamasishana kushiriki kwa amani na utulivu kwa maana nchi ni yetu na hatuna mbadala wake” amesema Manko katibu tawala wilaya ya Bariadi.

Naye mwenyekiti wa watuma salamu taifa Abubakari Sendeu ambaye ametetea kiti chake ameiambia Jambo FM kuwa hatua ya uchaguzi inayofikiwa kila baada ya miaka mitatu na umoja huo inaonyesha ukomavu wa chama hicho wa kuachiana madara kwa amani na kuwataka watuma salamu kote nchini kuona uchaguzi huo kama mwanzo wa kushiriki uchaguzi mkuu kwa njia ya amani.
“Tunatekeleza uchaguzi kwa mujibu wa katiba yetu kama watuma salamu na ninaamini kwa nguvu tuliyonayo watuma salamu tunakwenda kuitumia kuhamasishana kila pembe ya nchi tuweze kufanya uchaguzi mkuu kumchagua Rais ,wabunge na madiwani kwa njia ya amani na upendo” Amesema Sendeu
Awali kabla ya kufanyika uchaguzi huo washiriki wa kongamano hilo wametembelea hospitali ya halmashauri ya mji wa Bariadi na kufariji wagonjwa kwa zawadi mbalimbali kama njia ya kuonyesha upendo na kuguswa na mitihani wanayoipitia sambamba na kuwaombea dua warejee afya zao haraka.
“Tumefika hapa na zawadi chache kuwafariji na kuwaombea mrejee afya zenu haraka huku tukiamini huu ni mtihani mnapitia na mngetamani kuendelea na majukumu yenu kama siku zote lakini Mungu amepanga hivi,kwa hizi zawadi chache tunaomba mzipokee na muamini kuwa tuko pamoja” Lenga Chapati makamu mwenyekiti watuma salamu.
Akipokea zawadi hizo mganga mfawidhi wa hospitalii hiyo Rosemary Mushi amewashukuru watuma salamu kwa kujitolea kwao huku akiwataka watanzania wengine kuguswa na tukio hilo.
“Kipekee nitoe shukrani kwa niaba ya wagonjwa mtakao wafikia kwa siku ya leo na pia nitoe wito kwa watanzania wengine kuguswa na tukio hili kwani hawa wagonjwa ni ndugu zetu ambao tunafaa kuwafariji kwa kila hali” amesema Rosemary
Kongamano la watuma salamu limekamilika kwa kufanyika uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa chama hicho ambao utadumu kwa muda wa miaka mitatu hadi 2028 kwa mujibu wa katiba yao.



One response to “KONGAMANO LA WATUMA SALAMU KITAIFA LAFANYIKA SIMIYU, HIKI WALICHOKIAMUA..”
Mimi Abubakary sendeu mwenyekiti wa Umoja wa Wanasalamu Tanzania nakupongeza wewe mtangazaji Sada Almasi pia uongozi wa Jambo Boss Bizzo