Kodi Yakwamisha Misaada Kuingia Sudani Kusini

Umoja wa mataifa wasema malori yanayosafirisha bidhaa za misaada ya kibinadamu zinazohitajika kwa kiasi kikubwa nchini Sudan Kusini, yamekwama kwenye mabohari na kivuko cha mpaka kutokana na mzozo wa kodi.

Wiki hii, wizara ya biashara nchini humo ilianzisha ushuru mpya wa dola 300 kwa kila lori linalosafirisha bidhaa ndani au nje ya nchi hiyo ikiwa ni katika harakati za kuongeza mapato.

UNMISS imesema kutokana na hatua hiyo, serikali ilikuwa bado haijatoa kibali cha kuvuka kwa malori hayo yaliyokodishwa na Umoja huo wa Mataifa yaliyokuwa yamepakia mafuta kutoka nje licha ya kuhakikishiwa kuwa yamesamehewa kulipa kodi.

Kaimu msemaji wa UNMISS  Priyanka Chowdhury ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanaendelea kufanya mashauriano na maafisa wa ngazi za juu ili kutatua suala hilo.

Misheni za kidiplomasia zimepinga hatua hiyo, huku zikitoa wito wa kuondolewa kwa ushuru huo dhidi ya mashirika ya kibinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *