Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amezindua rasmi Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa huo, kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Huduma hizo zilizozinduliwa hii leo Januari 21, 2024 zitatolewa katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi Moshi Mkoani Kilimanjaro, kuanzia Januari 21 – 27, 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Kliniki hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Babu ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Kilimanjaro ili kutoa huduma ya Kliniki bure kwa wananchi.
Amesema, “tunaishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kutoa huduma hii bure kwa wananchi wetu hii inaonyesha namna Ofisi hii ilivyojikita kusogeza huduma kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini.”
RC Babu ameongeza kuwa, Kliniki hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya Wanachi dhidi ya Serikali, zitawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria, pia zitawasaidia Mawakili wa Serikali kushirikiana kwa ukaribu na Wadau pamoja Wananchi katika kutatua masuala ya Kisheria.
“Leo tunakwenda kuanza Kliniki ya Sheria ni matumaini yangu itawasaidia wananchi wenye matatizo ya kisheria, kuna timu nzuri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakuwa inatatua changamoto mbalimbali za wananchi,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tamari Mndeme amesema wamejipanga vyema kutoa huduma za Kisheria bure kwa wananchi.
Kliniki ya Sheria bila malipo ni mwendelezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za Kisheria kwa Wananchi.