
Na Melkizedeck Antony,Mwanza
Mkazi wa Nyakato mkoani Mwanza, Bashiri Mohamed (35), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza akikabiliwa na shtaka la kufanya mapenzi na mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 16.
Akisoma shtaka hilo jana tarehe Mei 21,2024 mwendesha mashtaka wa serikali Mwanahawa Changale amesema Mshtakiwa kwa tarehe tofauti kuanzia Septemba 2023 hadi Februari 15, 2024, eneo la Nyakato-Mecco, wilaya ya Ilemela anadaiwa kufanya mapenzi na binti huyo (16) huku akitambua ni mtoto wake wa kumzaa.
Changale amesema mshtakiwa ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 158 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022, hata hivyo, baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa amekana shtaka na kuomba apatiwe dhamana.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, wa mahakama hiyo Juma Opudo amemtaka mshtakiwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili watakosaini hundi ya maneno ya Sh 4 milioni kila mmoja na mwingine awe na mali isiyohamishika.
Hata hivyo, mshtakiwa amekwama kutimiza masharti ya dhamana kwani barua ya udhamini ya mdhamini mmoja aliyetokea wilayani Magu haikuthibitishwa na Hakimu Mfawidhi wa wilaya yake.
Hakimu ameahirisha Shauri hilo hadi Juni 11, mwaka huu litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kusomewa hoja za awali.