Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali imejipanga kuanza kubangua korosho ndani ya nchi kwa kujenga kiwanda cha kubangua korosho mkoani Mtwara pamoja na lindi ili ziweze kuuzwa zikiwa zimebanguliwa lengo ikiwa ni kupata faida kwa kupandisha bei zaidi ya zao hilo.
Rais Samia amesema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa katika ziara yake ya kikazi mkoani lindi na kuongeza kuwa jambo hilo litasaidia kupandisha bei ya zao la korosho na mazao mengine yanayopatikana mkoani humo.
Aidha rais Samia amewataka wakulima wote nchini kuitumia vizuri fursa ya pembejeo za mazao zinazotolewa bure na serikali kwa kutunza fedha kwa ajili ya matumizi ya baadae ya kilimo na kuwa na uwezo wa kutosha wa kununua pembejeo na mbolea pale ambapo serikali itasitisha zoezi hilo.
Hata hivyo rais Samia amesema kuwa serikali itaendeleza zoezi la utafiti katika sekta ya madini ili kutambua kiasi cha madini kinachopatiakana nchini pamoja na kuwatengenezea mazingira mazuri wachimbaji wadogo wa madini kuchimba kitaalamu zaidi pamoja na kuinua kipato chao