KIPINDUPINDU CHAUA WATOTO WANNE WA FAMILIA MOJA SIMIYU.

NA SAADA ALMASI -SIMIYU

Kufuatia ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo mbalimbali mkoani Simiyu, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza mapambano ya Kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo. 

Mapambano hayo yamehusisha viongozi wa kata ya Somanda wakishirikiana na shirika la SMV lilalojishughulisha na mabadiliko ya tabia ya nchi ambalo lipo katika mradi wa Ujenzi wa vyoo katika kaya 1000 ambapo wametoa elimu iliyokwenda sambamba na Bonanza maalum la kuendesha baiskeli katika Mtaa wa Nyamimbi kata ya Somanda Wilayani Bariadi mkoani Simiyu huku wakileta vyoo vya mfano na vinavyojengwa kwa gharama nafuu na salama ili kutoa hamasa kwa wananchi kujenga ,kutumia ili Kujikinga na maambukizi ya Kipindupindu.

Akizungumza kwenye mkutano na Wananchi, Afisa mtendaji wa kata ya Somanda, Daniel Moses amesema ‘Tumepata taarifa Watoto wanne wa Familia moja na wasio na hatia wamefariki na si eneo la mbali na hapa sababu ni uchafu wa mazingira waliyokuwa wakiishi yaliyopelekea Kupata ugonjwa wa kipindupindu, tulione hili na tuwe makini kujikinga sisi na familia zetu” – Daniel.

Daniel Moses pia amekemea Tabia ya baadhi ya Wananchi kuendekeza mila potofu zinazomkataza mtu na mkwewe Kutumia choo kimoja akitaja mila hizo kupitwa na wakati “kuna utamaduni kwamba huwezi kutumia choo na mkwe ni aibu na imani potofu hapa ni Mjini na hivi sasa tunaelekea kuwa manispaa tubadilike, tuachane na mambo hayo nawataka tuhimizane kila kaya iwe na choo’ – Daniel.

Takwimu za Kitaifa hivi karibuni ziliutaja mkoa wa Simiyu kwa nafasi ya pili kutoka mwisho katika suala la usafi wa Mazingira hususan matumizi ya vyoo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *