KINANA NI KADA MTIIFU, MZALENDO – RAIS SAMIA

Mwenyekitiwa Chama Cha Mapinduzi – CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana ni mmoja wa makada watiifu wa CCM na mwenye uzalendo usiotiliwa shaka.

Dkt. Samia ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye Mkutano Mkuu maalum uliowakutanisha wanaCCM kwa ajili ya kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyokuwa wazi.

Amesema Kinana ambaye anapumzika baada ya kuitumikia CCM kwa muda mrefu katika nafasi mbalimbali za uongozi, amekitumikia Chama tangu wakati wa TANU hadi CCM na hata kabla ya mfumo wa vyama vingi Nchini.

“Katika kipindi chote hicho hadi leo, Ndugu Kinana amekuwa mmoja wa makada watiifu wa CCM na mwenye uzalendo usiotiliwa shaka kwa nchi yake. Amekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, mjumbe wa Kamati Kuu, Katibu Mkuu wa CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara,” alisema Rais Samia.

Ameongeza kuwa, mbali na utumishi wake ndani ya CCM, Kinana pia alikuwa ni mmoja wa Maaskari hodari aliyetumikia nchi yake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hadi kufikia cheo cha Kanali na pia aliitumikia nchi kwa nafasi mbalimbali Serikalini.

Rais Samia amesema, “Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa inamshukuru sana na kumpongeza kwa dhati Ndugu Abdulrahman Kinana kwa uongozi wake thabiti katika utumishi wake ndani ya CCM na Serikalini.Tunamtakia mapumziko yenye furaha, afya njema na umri mrefu, pamoja na kumhakikishia ushirikiano wetu kwake.”

Akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano huo, Kinana alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa wanaCCM na Mwenyekiti wa Chama hicho kwa kumuamini na kumteua katika awamu mbili tofauti za nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM.

Aidha, aliwashukuru wana CCM wote wakiwemo watangulizi wake katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti na kumpongeza Stephen Wasira kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti akisema ni mtu sahihi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *