Na,Ibrahim Rojala
Zoezi la serikali ya Namibia la kukusanya zaidi ya wanyapori 700 ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na ukame mbaya zaidi katika miongo kadhaa linaendelea, huku takriban wanyama 160 wakiwa wamechinjwa.
Namibia ilitangaza zoezi hilo wiki iliyopita ili kupunguza matumizi ya malisho na usambazaji wa maji, na kutoa nyama kwa ajili ya mpango wa kusaidia maelfu ya watu wanaokabiliwa na njaa kutokana na ukame.
Mpango huo unaotekelezwa na wawindaji wa kitaalamu, unalenga viboko 30, nyati 60, swala 50, tembo 83, nyumbu 100, na pundamilia 300 na hadi sasa takriban wanyama 157 kati ya 723 waliopangwa kuchinjwa wameuawa hadi sasa na kuwezesha upatikanaji wa kilo 56,875 za nyama.
Namibia ilitangaza hali ya dharura mwezi Mei kutokana na ukame, ambao umekumba nchi kadhaa za kusini mwa Afrika na Msemaji wa wizara ya Mazingira nchini Namibia Romeo Muyunda amesema Lengo ni kutekekeza operesheni hiyo kwa muda wa kutosha huku wakipunguza kiwewe kadri iwezekanavyo.