KILIMO.
Kilimo ni neno lenye maana pana inayojumuisha mifumo ya uzalishaji wa mimea mbalimbali, ama ufugaji wa wanyama na uvuvi wa samaki.
Hata hivyo, mara nyingi Kilimo cha Mimea huenda sambamba na ufugaji wa Wanyama kama vile Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo, Kuku nk.
Tanzania ni moja ya nchi zinazotegemea Kilimo kama chanzo cha mapato na chakula ambapo familia nyingi hijihusisha na ulimaji mazao mbalimbali karibu maeneo mengi nchini.

CHANGAMOTO.
Lakini, sekta hiyo muhimu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Wakulima wengi kukosa elimu sahihi ya mbinu bora za kilimo na matumizi mabaya ya ardhi.
Changamoto nyingine ni kushindwa kupambania na rasilimali za asili, udhibiti wa magonjwa ya mimea na na wadudu, mdororo wa kiuchumi na kibiashara.
Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kwamba upo umuhimu wa kuweka mkazo katika kuboresha Kilimo na kuhakikisha Wakulima wanatumia mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

KILIMO BORA.
Hii ni njia ya kilimo inayozingatia matumizi sahihi ya rasilimali za Kilimo na mbinu bora ambazo zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao wenye kuleta matokeo chanya.
Hatua hii, kuhakikisha Wakulima wanatumia mbinu bora za kilimo kulingana na aina ya udongo, hali ya hewa na mazingira husika kea lengo la kuleta ufanisi.
KANUNI.
Hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija na kusaidia kuboresha maisha ya wakulima na jamii kwa ujumla kwani huleta miongozo au taratibu za kisayansi zilizofanyiwa majaribio na kukubalika zitumike ili kuboresha uzalishaji.

Hizi huzingatia mambo mbalimbali kama vile matumizi sahihi ya ardhi, utunzaji wa mazingira, matumizi ya mbegu bora, kufuata kanuni za usalama, afya, uchumi nk.
ENEO LA KILIMO.
Uchaguzi wa eneo linalofaa na kuliandaa mapema ni jambo la kwanza na muhimu kabla ya kuanza mradi wowote wa kilimo.
Hatua hii humfanya mkulima achague maeneo yanayofaa kwa Kilimo kulingana na aina ya mazao anayotaka kupanda, hali ya hewa, mwinuko wa ardhi, na aina ya udongo.

Hivyo ni muhimu kuzingatia hatua hii endapo unataka mabadiliko katika uvunaji wenye tija wa mazao yako ambayo umedhamiria kuyahudumia ili uweze kupata mavuno bora yenye tija.
MUHIMU.
Uchaguzi wa eneo unatakiwa kuzi gatia udongo wenye rutuba na unaoweza kupitisha maji na hewa vizuri na lenye uhakika wa maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji.
Muhimu maji hayo yasiwe na chumvi au sumu ambazo zinaweza kuathiri mimea au afya ya watumiaji na eneo hilo liwe la tambarare au lenye mteremko mdogo, ili kurahisisha shughuli za kilimo kama kupanda, palizi, uvunaji na usafirishaji.

Uchaguzi wa eneo lisilo la tambarare huweza kusababisha mmomonyoko wa udongo au upotevu wa maji, lakini pia ni muhimu kuhakikisha linafikika kwa urahisi kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa pembejeo za kilimo.
Pia eneo atakalochagua Mkulima linatakiwa liwe salama, na wanyama waharibifu, magonjwa, wadudu au wezi ambao watahatarisha uzalishaji na usalama wa mkulima.
MAANDALIZI.
Maandalizi ya mapema ya shamba kabla ya msimu ni muhimu kwa uzalishaji wa mazao bora na mengi, kwani kutokuandaa mapema shamba kunaweza leta athari za kimafanikio kwenye msimu wa uzalishaji na kusaidia kupata mavuno mengi.

Uandaaji wa mapema wa shamba husaidia kudhibiti magugu kabla ya kupanda, kwa kukatua udongo hatua ambayo huondoa na kuzika mbegu za magugu, hivyo kupunguza umeaji wa magugu wa baadaye.
AFYA YA UDONGO.
Kwa kukatua udongo, masalia ya viumbe hai huchanganywa vizuri kwenye udongo, hivyo kuboresha muundo na rutuba ya udongo na kudhibiti Wadudu.
Pia kuandaa shamba mapema husaidia kudhibiti wadudu kwa kuharibu mzunguko wa maisha yao na kupunguza idadi yao, hali ambayo hufanya udongo kuwa wenye rutuba.

MBEGU BORA.
Ni muhimu Mkulima akazingatia maandalizi ya mbegu, mchakato amabo ni muhimu ili kuhakikisha kunakuwa na mbegu bora iliyo tayari kwa kupandwa.
Mbegu bora ni zile zilizozalishwa nchini au zimeletwa nchini kutoka nje ya nchi na kisha zikathibitishwa na mamlaka ya kudhibiti ubora wa mbegu nchini Tanzania, TOSCI.
Pia mbegu bora zinaweza kuzalishwa kutoka kwenye vituo vya utafiti wa kilimo vya serikali (TARI) au makampuni binafsi.

Ifahamike kuwa mbegu zinazozalishwa na vituo vya utafiti vya serikali, husambazwa na kuuzwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini, ASA.
MAZINGIRA.
Hii ni sehemu muhimu ya kilimo bora, ambapo Wakulima wanahimizwa kuhifadhi na kutumia rasilimali za asili kwa njia endelevu kwa kuhakikisha rasilimali kama maji, udongo, na bioanuai zinatunzwa na kutumiwa kwa njia ambayo haitaleta uharibifu wa mazingira.

HITIMISHO.
Kililimo ni uti wa mgongo katika Taifa la Tanzania, huu ni muhimili wa maendeleo ya kiuchumi, ukiajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wote, huku ikichangia karibu asilima 30 ya pato lote la Taifa.
Hivyo ni muhimu kufanya Kilimo kisicho cha mazoea na utegemezi, na badala yake tujikite katika kilimo cha biashara chenye tija kwa Taifa na pato la mtu mmoja mmoja.