Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuhakikisha huduma ya afya inawafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao.

Majaliwa ameyasema hayo akizungumza kama mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Itilima wilayani Itilima mkoani Simiyu Februari 15, 2025, ambao ulilenga kuwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020/25 jimboni humo.
Majaliwa ameeleza kuwa wilaya ya Itilima tayari ina zahanati 37, na lengo ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati yake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

“Tunataka mwananchi apate huduma za afya karibu na makazi yake. Hongera sana Mheshimiwa Njalu Silanga (Mbunge wa Itilima) kwa kuhakikisha wilaya hii inapata zahanati nyingi. CCM itaendelea kuhakikisha mbunge wenu anapata ushirikiano wa Serikali ili huduma zote zipatikane hapa Itilima,” amesisitiza.