Bibi mmoja aitwaye Malogi Mwaihoyo(75) mkulima na mkazi katika kijiji cha Ikoho kilichopo wilayani Mbeya anashikiliwa na polisi Mkoani Mbeya kwa kosa la mauaji ya mjukuu wake aitwaye Vision
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga mauaji hayo yalitokea Agosti 31 mwaka huu majira ya saa nne na nusu asubuhi katika Kitongoji cha Mapinduzi Kijiji cha Ikoho, Kata ya Maendeleo ambapo asubuhi hiyo bibi huyo aliamkia kazi ya kuchimba udongo kwaajili ya maandalizi ya kukandika nyumba yake akiendelea kusafisha eneo kwa kutumia jembe alisikia sauti ya mtoto mdogo akilia kwa nguvu baada ya kushusha jembe ardhini pasipo kujua wakati anaendelea na kazi yake mjuu wake alikuwa amekwisha tambaa akimfuata hadi eneo alilokuwa akiendelea na kazi na ndipo alijikuta amemshushia jembe kichwani na kumfanya apoteze uhai wake.
Kamada huyo anabainisha kuwa uchunguzi wa awali ulionesha bibi huyo ana tatizo la uoni hafifu yani akikabiliwa na upofu hivyo kwa haraka hakuweza kujua pale chini kuna nini na ndiyo sababu hata aliposikia sauti alilazimika kuuliza watu waliokuwa jirani kuwa kulikuwa na nini na ndiyo waliomwambia amemkata mjukuu wake na amefariki.
Alisema kikongwe huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi wakati taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kufanyika.