Mchezaji Khalid Aucho wa klabu ya Yanga amefungiwa michezo mitatu na
kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji
Ibrahim Ajibu wa klabu ya Coastal Union katika mchezo.
Adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni ya 41:5(5.3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti
kwa Wachezaji.
Klabu ya Coastal Union imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa
kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka nje ya chumba cha kuvalia, jambo
lililosababisha mchezo huo kuchelewa kuanza kipindi cha kwanza na baada ya
mapumziko, hivyo kuharibu programu za mrusha matangazo ya runinga (Azam
TV) ambaye ni mdhamini mwenye haki za matangazo ya runinga.
Adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni ya 17:60 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za
Mchezo.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Emmanuel Mwandembwa
(Arusha) amefungiwa kwa miezi sita (6) kufanya kazi ya uamuzi wa mpira wa
miguu, kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za mpira wa miguu
jambo lililosababisha ashindwe kumudu mchezo tajwa hapo juu.
Adhabu hii kwa kuzingatia kanuni ya 42:1(1.1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa
Waamuzi.
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imefuta kadi ya manjano
aliyoonyeshwa mchezaji Semfuko Charles wa Coastal Union (37) baada ya
kujiridhisha kuwa mchezaji huyo hakustahili adhabu hiyo.
Uamuzi huu ni kwa kuzingatia kanuni ya 12:8 ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa
Ligi.