KESI YA UHAINI: LISSU AWATAJA MASHAHIDI WAKE

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amewataja Mashahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili ambayo inaendelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dar es Salaam.

Mbele ya Mahakama, Lissu amesema Shahidi wake wa kwanza ni Samia Suluhu Hassan ambaye anapatikana Ikulu ya Kivukoni.

Amesema, “Shahidi wangu wa kwanza ni Samia Suluhu Hassan. Anapatikana Ikulu ya Kivukoni. Akikosekana anapatikana Ikulu ya Dodoma.”

Lissu ameongeza kuwa, “Shahidi wangu wa 2 anaitwa Philip Isdor Mpango. Huyu anapatikana ofisi ya makamu wa Rais, mji wa Serikali Dodoma. Shahidi wangu wa 3 anaitwa Kassim Majaliwa Kassim. Huyu anapatikana ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.”

“Shahidi wangu wa 4 anaitwa Inspector General of Police (IGP), Camillus Wambura. Huyu anapatikana makao makuu ya polisi Dodoma. Shahidi wangu wa 5 anaitwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ramadhani Kingai. Huyu anapatikana ofisi ya makao ya polisi Dodoma,” aliendelea Lissu.

“Shahidi wa 6 ni Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Huyu simfahamu jina. Lakini anapatikana yalipo makao makuu ya usalama wa Taifa. Shahidi wangu wa 7 anaitwa Kamishna wa Polisi (DCP) Ramadhani Ng’anzi. Huyu anapatikana makao makuu ya polisi Dodoma,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Shahidi wangu wa 8 anaitwa Agather Atuhaire. Huyu yupo Kampala, Uganda. Yule aliyetekwa nyara na kuteswa na kwenda kutupwa mpakani. Shahidi wangu wa 9 ni Boniface Mwangi. Huyu yupo Nairobi, Kenya. Huyu alitekwa nyara, akateswa na kwenda kutupwa mpakani Horohoro.”

“Shahidi wangu 10 atakuwa John Marwa. Huyu ni Mkurugenzi wa Jambo TV. Shahidi wangu wa 11 atakuwa Amani Sam Golugwa. Huyu ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA. Huyu anajua mkutano huo uliitishwaje,” aliendela Lissu.

“Shahidi wangu wa 12 ni John Wegesa Heche, huyu ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA. Anajua nilikuwa wapi kipindi hicho. Shahidi wangu wa 13 atakuwa John John Mnyika. Huyu ni Katibu Mkuu wa CHADEMA. Ofisi yake ni Makao Mkuu ya CHADEMA. Shahidi wangu wa 14 atakuwa Dr. Willy Munyoki Mutunga anapatikana Nairobi, Kenya,” aliongeza Lissu.

Aidha amemaliza kwa kusema, “Shahidi wangu wa 15 atakuwa ni Martha Wangari Karua. Huyu anapatikana Nairobi, Kenya. Naomba nihifadhi haki yangu ya kuwaita mashahidi wa ziada kama hawa hawatatosha.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *