Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassor Katuga amesema upande wa Jamhuri umefunga ushahidi kwa shahidi wa 17 katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Uamuzi huo, umefikiwa baada ya Jamhuri kufanya tathmini ya kina ya ushahidi na hoja zote, zilizowasilishwa katika kesi hiyo inayoendelea mbele ya jopo la Majaji watatu likiongozwa na Dastan Ndunguru.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalohusishwa na maneno aliyodaiwa kuyatamka kuhusu kusudio la kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hata hivyo, Katuga ameiomba Mahakama iruhusu Jamhuri kuwasilisha hoja za ziada kueleza sababu zinazowafanya waone Lissu ana kesi ya kujibu, ombi ambalo Lissu amepinga akieleza kuwa sheria tayari inaweka utaratibu unaopaswa kufuatwa katika hatua hiyo.
Endapo Mahakama itaona Lissu ana kesi ya kujibu, atapewa nafasi ya kuanza kujitetea kwa kuwasilisha ushahidi na Mashahidi wake na kama hatakuwa na la kujibu, kesi hiyo itakuwa imefikia mwisho.


