
Rais wa Kenya, William Ruto amesema kwamba Kenya imepeleka rasmi ombi la kuandaa Tuzo za Grammy na tayari imelipa kiasi cha Kenya Shilingi milioni 500 ili kufanikisha maandalizi ya tuzo hizo.
Katika kuadhimisha mwaka wa pili wa Serikali ya ‘Hustler’ kwenye mkutano wa hadhara katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC), Rais Ruto alisitiza kujitolea kwa utawala wake katika kuimarisha tasnia ya ubunifu ya Kenya na kuiweka nchi kama kitovu cha burudani ulimwenguni.

Mwezi April, Rais Ruto alisema kuwa Kenya imechaguliwa kuwa mojawapo ya nchi nne zitakazoshiriki katika tuzo za Grammy kupitia ushirikiano na Grammy Global Ventures.Ushirikiano huu unatajwa kuimarisha ushiriki wa Kenya katika tasnia ya ubunifu ya kimataifa.
Wakati wa tangazo hilo, Rais Ruto alisisitiza umuhimu wa kujumuisha sanaa ya maonyesho katika mfumo wa elimu wa Kenya na kupendekeza kuunda mitaala maalum ya mafunzo kwa waelimishaji wa sanaa na akasisitiza mipango muhimu kama vile Idara ya Uchumi Ubunifu na Talanta Hela, ambayo inalenga kukuza na kuchuma talanta za ndani.
Pia alitaja ushirikiano ujao na Hollywood kusaidia tasnia ya filamu nchini Kenya na kuwapa wabunifu wa ndani fursa ya masoko ya kimataifa.
Wakati huo huo, Dennis Itumbi, Mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Uchumi wa Ubunifu, alifichua Jumatatu kwamba ofisi yake iliagiza Idara ya Mambo ya Nje kuwezesha malipo ya jitihada za Kenya kuandaa Tuzo za Grammy za Afrika.
Dennis Itumbi alisema pia kuwa serikali ya Kenya inataka kuandaa Kongamano la Dunia la Uchumi Ubunifu mnamo 2027, hatua ambayo itafanya Kenya kuwa taifa la kwanza la Kiafrika kuandaa hafla hiyo ya kifahari.
“Tayari nimemwandikia Rais barua kwa niaba ya Ofisi ya Kuratibu Uchumi Ubunifu, nikipendekeza kwamba Kenya ianze rasmi azma yake ya kuandaa Kongamano la Kimataifa la Uchumi Ubunifu mwaka wa 2027,” alisema Itumbi.


