Na Daniel Gahu – Katavi.
Serikali ya Mkoa wa Katavi imepokea timu maalum kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Kwa lengo la uzinduzi wa zoezi la kutoa huduma ya chanjo na utambuzi wa mifugo yote iliyopo ndani ya Mkoa.
Timu hiyo imehusisha Madaktari wa mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wataalamu wa Tehama ambao wamefanya kazi kwa kushirikiana na watendaji wa Mkoa wa Katavi ambapo uzinduzi huo umefanyika katika halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe kata ya Maji moto.

Zoezi hilo lililozinduliwa na ndugu Tolokolo Kayumba Kwa niaba ya Katibu tawala wa Mkoa wa Katavi amesema mbele ya wafugaji kuwa ujio wa zoezi hilo ni katika kutekeleza maono na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alipozindua kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo yote Kitaifa mnamo tarehe 16 June, 2025 Mkoani Simiyu.
Daktari mbobevu wa Mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi ndugu Moses Mambene amesema awamu hii ya kwanza Kwa Mkoa wa Katavi utalenga uchanjaji wa chanjo kwa mifugo zaidi ya laki nane kwa ng’ombe, mbuzi zaidi ya laki tatu huku kitaifa wakitarajia kuchanja mifugo milioni 19.1 Kwa chanjo tano ambapo ni chanjo ya homa ya mapafu ya Ng’ombe huku Kwa mbuzi na Kondoo itahusisha chanjo ya Sotoka, Mdondo,Ndui pamoja na mafuta ya kuku.

Pia amesema, Kwa upande wa utambuzi wanatarajia kuvisha hereni mifugo yote ambayo itakuwa imechanjwa ukiondoa mifugo ya kuku, huku akibainisha chanjo zote zitatolewa bila malipo yoyote kwani Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya usimamizi wake Daktari Samia Suluhu Hassan imeshakwisha kutoa ruzuku ya asilimia mia Moja Kwa chanjo hizo.
“Zoezi hili la kutoa huduma ya chanjo kwa mifugo ni bure kabisa hivyo niwahamasishe sana wafugaji walete mifugo yao ili ipatiwe chanjo pamoja na kutambuliwa” amesema Daktari Mambene huku Wafugaji wao wakimshukuru Rais kwa kuwaletea huduma hiyo ya chanjo bila malipo.

Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na rasilimali kubwa ya mifugo pamoja na wingi wa rasilimali hizo mchango wake katika pato la Taifa ni asilimia 6.2. Ambapo moja ya sababu za mchango huu kuwa mdogo ni pamoja na uwepo wa magonjwa ya mifugo yanayosababisha vifo na kuathiri biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.
Kutokana na umuhimu wa mazao ya mifugo Serikali iliandaa mpango wa chanjo na utambuzi wa mifugo yote Kitaifa Kwa miaka mitano 2024/2025 – 2028/2029. Ambapo Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi 216,140,097,000 Kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mpango huu ambao hadi hivi sasa umeanza rasmi Kwa mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Dar es Salaam.


