KATAVI YAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MIAKA 4 YA URAIS.

Na Gideon Gregory, Dodoma

Katika kuhakikisha mkoa wa Katavi unaendelea kuimarika kiuchumi, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali, hususan barabara, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya ndani ya mkoa huo.

Hayo yameelezwa leo Juni 3, 2025 na Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko wakati akizungumza na waandishi wa habari hapa Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya mkoa huo katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Maboresho haya ya sekta ya miundombinu hii ya barabara lakini na miundombinu mingine ya usafirishaji imiweza kuleta mafanikio makubwa, nikigusia sekta ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali tumeweza kukusanya zaidi ya Bilioni 118 katika kipindi hiki cha takribani miaka minne na nusu ambayo ni zaidi ya asilimia 100 ya malengo yaliyokuwa yamewekwa,” amesema.

Aidha, Mkuu huyo amesema ujenzi wa shule hizo mpya umewapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu pamoja na  msongamano wa wanafunzi madarasani ikiwa ni pamoja na kuwezesha mazingira bora zaidi kwa wanafunzi na walimu.

“Kwa kipindi cha uongozi wa Rais wa awamu ya sita, Sekta ya Elimu imepokea kiasi cha Shilingi 58,093,065,268.19 zilizotumika katika kuboresha miundombinu ya Shule mbalimbali na kuweka mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunza.

“Pamoja na Ujenzi wa Shule mpya mia thelathini na saba zikiwemo Shule 97 za Msingi na Shule 40 za Sekondari, madarasa 2,219 madarasa ya awali 6, matundu ya vyoo 2,734,” amesema.

Katika sekta ya Afya  Mkuu huyo amesema mkoa huo umepokea zaidi ya Tsh.Bilioni 41 kwa ajili ya kuboresha huduma za Afya,ununuzi wa vifaa na vifaa Tiba,ujenzi wa Hospitali nne za wilaya,ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa,ujenzi wa vituo vya Afya 11 na ujenzi wa zahanati 47.

Pia amesema  zaidi ya Bilioni 196 zimepelekwa katika sekta ya Nishati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo upanuzi wa mtandao wa umeme kwa Wilaya ya Mpanda,Tanganyika na Mlele ambapo hadi sasa Vitongoji 504 kati ya Vitongoji 912 vya Mkoa wa katavi vimeunganishiwa umeme.

“Mkoa wa Katavi umeendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) ambapo Mwaka 2021 Mkoa ulikuwa na jumla ya vituo 102 vya kutolea huduma za Afya na hadi kufikia Mwezi Juni, 2025 Mkoa una Jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya 161 ikiwa ni ongezeko la vituo 59, Sawa na ongezeko la asilimia 36.64,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *