Na Daniel Gahu – Katavi.
Kufuatia kasi ya ukuaji wa Sayansi na Teknolojia ulimwenguni, wadau wa elimu katika Kata ya Sitalike wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Ndugu Athman Juma Fimbo wamekabidhi vifaa vya TEHAMA katika shule za msingi na sekondari katika Kata ya Sitalike.
Akikabidhi vifaa hivyo akiwa katika makao makuu ya Kata ya Sitalike, Fimbo amesema ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ameona umuhimu wa kuiunganisha Kata ya Sitalike na Ulimwengu kupitia vifaa vya TEHAMA huku akianza na taasisi za elimu katika Kata hiyo.

Amesema, utoaji wa vifaa hivyo umeenda sambamba na ahadi yake aliyoitoa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akisisitiza kuendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma katika jamii.
“Leo hii nimekabidhi vifaa vya TEHAMA ikiwa ni kompyuta pamoja na Projekta, kwa shule zetu zote za Kata ya Sitalike kwa lengo la kuhakikisha tunaboresha elimu kwa watoto wetu na kuweza kuwa wa kisasa zaidi kwa dunia hii inavyokwenda,” amesema Fimbo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Sitalike Yusuph Shitindi amesema atashirikiana na Walimu kuhakikisha vifaa vilivyokabidhiwa vinatunzwa vizur ili viweze kudumu na kusaidia vizazi vijavyo.
Aidha, baadhi ya walimu waliopokea vifaa hivyo vya TEHAMA wamewashukuru wadau na serikali kwa ujumla kwa kuwapatia vifaa vya TEHAMA, ili kuoboresha elimu huku wakiwa na matarajio ya kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji katika shule hizo.

Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sitalike Mwl. Charles Tekere amesema kama shule tunashukuru kwa utekelezaji wa ahadi hii ambayo ilitolewa wakati wa mahafali ya kidato cha nne mwaka 2025, huku akibainisha wazi changamoto walizokuwa wakipitia katika ufundishaji kutokana na ukosefu wa projekta.

Vifaa hivyo vya TEHAMA ikiwemo kompyuta na Projekta vyenye thamani ya takribani shilingi milioni sita za kitanzania vimekabidhiwa kwa shule za msingi na sekondari katika Kata ya Sitalike.

