KATAVI MGUU SAWA MAPAMBANO DHIDI YA KICHAA CHA MBWA

Na Daniel Gahu – Katavi.

Kichaa cha Mbwa ni maambukizi ya virusi hatari ambayo husababisha kuvimba kwa Ubongo na Uti wa mgongo kwa watu na wanyama, ambapo pia hutambulika kwa jina la kitaalamu kama Hydrophobia, ambayo ni maambukizi ya papo hapo na mabaya.

Katika kuhakikisha maambukizi ya virusi hatari ya kichaa cha Mbwa Mkoani Katavi, Serikali ya Mkoa imeadhimia kuhakikisha kila mfugaji wa Mbwa na Paka anawachanja wanyama hao ili kuzuia hatari ya wanyama kuvamiwa na maambukizi ya virusi vya kichaa cha Mbwa.

Serikali ya Mkoa kupitia kwa Afisa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ndugu Ezediel Mhando, ametanabaisha Mkoa wa Katavi una jumla ya Mbwa 28,000 na Paka 4,976 ambayo ni idadi kubwa na kupelekea kupokea visa vya matukio mbalimbali ya binadamu kung’atwa na Mbwa.

Taarifa hiyo imebanisha kuwa, kwa mwaka 2023 Mkoa wa Katavi ulipokea visa 188, Mwaka 2024 ulipokea visa 136 na Mwaka 2025 ulipokea visa 108 ambapo visa vya binadamu kung’atwa na Mbwa vimeonekana kupungua kutoka Mwaka hadi Mwaka, hiyo ni kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mkoa kudhibiti virusi vya kichaa cha Mbwa kwa kutoa chanjo hiyo bure kwa wafugaji pamoja na kuwapatia elimu Stahiki.

“Tathimini imebaini waathirika wakubwa wa kung’atwa na Mbwa ni watoto wadogo ambapo imechukua asilimia  64.3 kuwa waliong’atwa na Mbwa ni watoto wadogo,” amesema Mhando.

Aidha, amewashukuru wadau mbalimbali wanaoshirikiana na Serikali dhidi ya kutokomeza virusi vya kichaa cha Mbwa na kusema kutokana na juhudi za uchanjaji wa chanjo kwa mbwa, kumeupa nafasi ya kwanza Mkoa wa Katavi.

Ni Mkoa pekee hapa nchini unaochukua tahadhari na mapambano dhidi ya kichaa cha Mbwa sambamba na Kuifanya nchi ya Tanzania kushika nafasi ya tisa duniani kwa kuchukua hatua za mapambano dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha Mbwa.

Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Florence Chrisant ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua za mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa kichaa cha Mbwa kwa kuipeleka mifugo yao ya Mbwa na Paka katika vituo vilivyoidhinishwa na Serikali ya Mkoa ili iweze kupatiwa huduma ya chanjo na ushauri wa kitaalam kutoka kwa madaktari wa mifugo jinsi ya ufugaji bora wa wanyama hasa wa nyumbani.

“Niwaombe muichanje mifugo yenu ili kupunguza madhara kwa jamii dhidi ya magonjwa yatokanayo na kichaa cha Mbwa, kwani mtu aking’atwa na akapata maambukizi ya virusi hatari ya kichaa cha Mbwa kutapelekea kudhorotesha shughuli za uzalishaji na kushuka kwa uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla” amesema Chrisant.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *