Na Daniel Gahu – Katavi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),, Mkoa wa Katavi, Iddi Hassan Kimanta amefanya ziara ya kikazi katika kata ya Ibindi iliyopo halmashauri ya Nsimbo kwa lengo la kuwashukuru wana CCM kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upigaji wa kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Amebainisha kuwa Mkoa wa Katavi ni moja ya Mkoa ambao ulitoa kura nyingi za mgombea wa nafasi ya Urais jambo lililopelekea kupata idadi kubwa ya wabunge wa viti maalum kwa kupata wabunge watatu ambao wamepata nafasi ya kuwa wawakilishi wa wananchi katika bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amewapongeza wananchi wa Kata ya Ibindi kwa kumchagua diwani makini na mwenye uchungu kwa wananchi wake katika suala zima la maendeleo.
“Niwe muwazi kwenu wananchi wa Ibindi kwa diwani huyu mmelamba dume hasa, maana miradi mingi ya maendeleo inaenda kasi kutokana na ufuatiliaji wake” amesema Comrade Kimanta.

Amewataka wanachama na viongozi wote kushikamana na kila mmoja awajibike kulingana na nafasi yake ili waweze kutimiza malengo ya ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa kwa ujumla.
Pia amehimiza swala zima la ulipaji wa ada kwa wanachama wote, huku akibainisha kuwa chama hakiwezi kuendeshwa pasipokuwa na pesa, ulipaji wa ada kwa wanachama ndicho kipimo sahihi cha uhai wa chama na wanachama.

“Unakuta mtu kwa siku anakunywa soda zaidi ya moja, wakati huohuo kiwango cha kulipia ada ni sawa na soda mbili za Shilingi mia sita sita hivyo mimi binafsi simuoni mwanachama hata mmoja ambaye hana uwezo wa kulipia ada” amesema Comrade Kimanta.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Ibindi Mdakuni Ramadhani Matongo amesema kata ya Ibindi itakuwa mstari wa mbele katika ufuatiliaji wa miradi ya Maendeleo na kubainisha yeye kama mwakilishi wa wananchi ndani ya kata kipekee atahakikisha miradi yote ambayo imeanzishwa na Serikali na ambayo itaanzishwa kwa nguvu za wananchi zote zinakamilika kwa wakati.

“Tunao mradi ujenzi wa kituo cha Afya cha kata, hadi hivi sasa kipo katika hatua ya mwisho ya kuweka madirisha ya aluminium, pia tunao mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na choo cha kisasa katika shule ya msingi Muungano ambapo hadi hivi sasa yapo katika hatua ya mwisho ya kuweka marumaru pamoja na mradi wa ujenzi wa josho la Mifugo ambalo nalo liko katika hatua za mwisho za ukamilikaji,” amesema Diwani Mdakuni.





