Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amesisitiza dhamira ya Mahakama ya Tanzania katika kufanya maboresho ya mifumo na miundombinu ya utoaji wa haki, ikijumuisha matumizi ya teknolojia ya kisasa inayokwenda sambamba na maendeleo ya kidijitali nchini.
Ametoa msimamo huo wakati wa mafunzo maalum yaliyowakutanisha Tume ya Mahakama na Kamati za Maadili za Wilaya na Mkoa wa Katavi, ambapo amebainisha kuwa maboresho hayo yanakusudia kuongeza ufanisi, uwazi na kupunguza changamoto katika mfumo wa utoaji wa haki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ameomba kuharakishwa kwa ujenzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika mkoa huo, akieleza kuwa wananchi wamekuwa wakilazimika kusafiri kwenda mikoa ya jirani kupata huduma hizo, jambo linalosababisha usumbufu na ucheleweshaji wa haki.

Amefafanua kuwa ongezeko la mashauri yanayohitaji kusikilizwa katika Mahakama Kuu ni miongoni mwa sababu zinazoongeza uzito wa hoja hiyo, akibainisha kuwa uwepo wa mahakama hiyo utasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza mzigo kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa huduma za kimahakama mkoani humo.
Aidha, mafunzo hayo yamelenga kuitambulisha Tume ya Mahakama kwa kamati za maadili pamoja na kuwaelekeza wajumbe wa kamati hizo kuhusu namna bora ya kushughulikia masuala ya kisheria na maadili katika maeneo yao ya kazi.

Afisa wa Sheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Lazaro Dotto ameueleza mchango wa kamati hizo katika kutoa elimu kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali, akisema kuwa elimu hiyo ni endelevu na itaendelea kutolewa kadri fursa zinavyojitokeza, kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa kuhusu kamati hizo na namna ya kuzitumia ipasavyo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Mahakama Mkoa wa Katavi, Thomas Ngozi, amepongeza hatua ya kuandaliwa kwa mafunzo hayo na ameeleza kuwa yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo wa kitaalamu wajumbe wa kamati hizo, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia maadili.