KASSIM AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA MTOTO

Na Saada Almasi – Simiyu.

Mahakama ya wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imemhukuku kifungo cha miaka 30 jela Kassim Masagyo Mwiburi (50) mkazi wa kijiji cha Njiapanda ya Malampaka wilayani humo kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 11.

Katika shauri hilo la jinai lenye namba 6282/2025 mshtakiwa alikutwa na hatia baada ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya hiyo Aziz Khamis kujiridhisha na ushahidi kutoka kwa mashahidi 5 waliofikishwa mahakamani hapo pamoja na vielelezo viwili.

Shauri hilo liliwasilishwa kutoka upande wa jamhuri na wakili wa serikali mwandamizi Suzan Msule pamoja na mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka wilayani humo mkaguzi msaidizi wa jeshi la polisi Vedastus Wajanga.

Ilidaiwa kuwa, Februari 26 mwaka 2025 mshtakiwa Kassim Masagyo Mwiburi alitenda kosa hilo majira ya usiku katika kijiji cha Njiapanda  kwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 11 mwanafunzi wa shule ya msingi ambaye majina yake yamehifadhiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto kinyume na kifungu cha (130)(1)(2)(e)na 131 cha sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022

Pamoja na kukamatwa kwake na jeshi la polisi mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na baada ya upelelezi kukamilika alipandishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Baada ya kutiwa hatiani upande wa mashtaka uliomba mshtakiwa apewe adabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye nia ya kufanya kitendo hicho ukizingatia vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji vinashika kasi katika jamii na kuacha makovu yasiyofutika.

Mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwani ni kosa lake la kwanza ndipo hakimu mkazi mwandamizi aziz khamisi wa mahakama hiyo akamhukumu kwenda jela miaka 30.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *