Kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 zimetangazwa rasmi kwenye gazeti la serikali na hivyo kuzipa nguvu ya kisheria zianze kutumika.
Hatua hii inairuhusu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuendelea na michakato mingine ya uchaguzi mkuu kwa vyama 18 vilivyosaini Aprili 12, 2025, jijini Dodoma.
Sehemu za kanuni hizo, zilizowekwa leo Aprili 18, 2025 zinavitaka vyama vya siasa na wagombea kutofanya fujo au kuchochea vurugu ya aina yoyote katika mikutano ya vyama vingine vya siasa.

Pia, kanuni inavitaka vyama vya siasa na wagombea wao kutotumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjifu wa amani au kuashiria ubaguzi wa kijinsia kwenye mikutano na kampeni zote.
Vyama vya siasa 18 vyenye usajili wa kudumu vilivyosaini kanuni hizi sasa vinapata nguvu zaidi ya kuendelea na michakato ya kiuchaguzi ya ndani huku wakisubiria utaratibu INEC.
Vyama vya CCM, ACT Wazalendo, NLD, ADC na vingine vilishaanza mchakato wa kuwatangaza wagombea watakaopeperusha bendera za vyama vyao. Uamuzi wa INEC, kuziweka kanuni hizo gazetini unawasha taa ya kijani kwa vyama hivi kuendelea na mchakato wa kuwapata na kuwarasimisha wagombea watakaosimama kwenye ngazi ya urais, ubunge na udiwani.

Miongoni mwa vyama vilivyopeleka makatibu wakuu wao kusaini kanuni hizo ni CCM, ADC, NCCR-Mageuzi, Chaumma, AAFP, Ada Tadea, Sau, CCK, TLP, Demokrasia Makini, DP, UPDP, CUF, NRA, UDP na UMD.
Kutokana na hilo, ni wazi Chadema haitaweza tena kushiriki uchaguzi mwaka huu na kulazimika kusubiri hadi 2030, kufuatia maamuzi yao wenyewe ya kutosaini kanuni hizi ambazo ni takwa la kisheria.
Kwa sasa maandalizi ya uchaguzi mkuu yanaendelea kupamba moto, yakiwaacha CHADEMA nje ya mchakato kwa kipindi cha miaka mitano.