Na Eunice Kanumba Shinyanga
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wamejadili taarifa ya hesabu za mwisho katika kipindi cha kuishia juni 2026, huku makampuni yanayodaiwa fedha za ushuru wa huduma ikiazimiwa kuwa yachukuliwe hatua.
Madiwani hao, wamejadili hayo katika mkutano baraza Maalumu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, uliopo katika kata ya Iselamagazi.

Akitoa salamu za mkoa katika baraza hilo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Ibrahimu Makana amesema, Makampuni yote ambayo yanadaiwa na Halmashauri hiyo yawasilishiwe taarifa zao kwenye Ofisi ya Mkoa, ili wachukue hatua.
Amesema, hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), linalotaka makampuni hayo kuwajibika kulipa ushuru huo.

Amemuagiza pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kuandaa mkakati wa kulipa madeni ambayo Halmashauri inadaiwa na wazabuni, pamoja na kuhakikisha halmashauri haizalishi madeni mapya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Seth Msangwa amesema, madeni ambayo Halmashauri inadaiwa na Watumishi ni muhimu yaanze kulipwa kwa kuanza na wastaafu.

Naye Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, CPA Shimi Emmanuel, amesema Shinyanga imeanza kupunguza madeni inayodaiwa, kutoka bilioni 1.9 hadi bilioni 1.7.
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kupitia baraza la Madiwani, imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundo mbinu pamoja na huduma za jamii kwa lengo la kuboesha maisha ya wananchi katika eneo hilo.




