KAMPENI ZA KITUMBO ZAPAMBA MOTO AKIAHAIDI NEEMA KATA YA MJINI

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Mgombea udiwani Kata ya Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Salum Kitumbo ameendelea na mkutano wa kampeni katika uwanja wa risasi uliopo katika Manispaa ya Shinyanga, huku akiaidi kutatua changamoto zote zilizopo katika kata hiyo, ikiwa ni pamoja kuleta jiko la kisasa na umeme katika shule ya msingi Mwenge.

Kitumbo pia ametumia jukwaa hilo kunadi sera kwa wananchi, ili ifikapo Oktoba 29 wamchague na awe diwani wao, pamoja na kumuombea kura za ushindi Dkt.Samia Suluhu Hassan na Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi.

Ameongeza kuwa, endapo akichaguliwa atahakikisha wazee katika kata hiyo ya mjini wanapatiwa bima ya afya ili waweze kupatiwa matibabu bure ili kuwapunguzia mzigo wa gharama za matibabu kwani umri wa uzee ndiyo kipindi ambacho mwanadamu ananyemelewa na magonjwa kwa wingi.

Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na kuhakikisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambao wamejiunga kwenye vikundi wanapata mikopo ya halmashauri asilimia 10 ili wapate kujikwamua kiuchumi.

Aidha, Kitumbo pia amewahidi vijana kuwa watanufaika na fursa ambazo hujitokeza katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kwa kupewa kipaumbele kwanza, ili wapate kujikwamua kiuchumi, ambapo kwa upande wa michezo, ameahidi kuinua sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha viwanja.

Nao viongozi mbalimbali wa Chama waliohudhuria mkutano huo, wamemuelezea Kitumbo kuwa ni kiongozi mzuri mwenye maono, pamoja na mpigania maslahi ya wananchi, kwamba Kata ya Shinyanga wamepata diwani ambaye ni kijana na mwenye ari ya kuwatumikia wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *