Halmashauri ya mji wa Geita imeanzisha kampeni ya nyumba kwa nyumba kuwasaka watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupelekwa shuleni na ambao walikatisha masomo kwa sababu mbalimbali warudishwe shuleni ili kutimiza ndoto zao.

Hayo yamebainishwa na afisa elimu msingi halmashauri ya mji wa Geita Zenaida Alphonce ambaye amesema kutokana na wazazi na walezi kuwaficha watoto wenye ulemavu wameamua kuanzisha kampeni hiyo ili kuwabaini watoto wote na mpaka sasa wamefanikiwa kuwafikia watoto zaidi ya 400. Kwa upande wao baadhi ya walimu wanaowafundisha watoto wenye mahitaji maalum wamesema uwepo wa kampeni hiyo imekuwa chachu ya kuhamasisha wazazi na walezi kuwaandikisha shule watoto wote wenye ulemavu na kuachana na na dhana potofu ya kuwaficha watoto ndani watoto hao.
Baadhi ya wazazi na walezi waliojitokeza kuwaandikisha watoto wao kuanza shule, wameipongeza halmashauri hiyo kwa kuja na kampeni hiyo kwani imewaibua watoto wengi huku wakiwataka wazazi na walezi kutokuwaficha watoto wao kwani wanawanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.