Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Wilaya ya Kahama imeendelea kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo katika sekta mbalimbali, huku madini kilimo na mifugo zikitajwa kuwa miongoni mwa sekta zinazoendelea kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hilo.
Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda wakati akieleza taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) katika wilaya hiyo na kuainisha kwamba wilaya hiyo inaendelea kusimamia kwa weledi utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusimamia fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Dc Nkinda amesema kwa ujumla, Kahama imepokea jumla ya Sh. 295,211,700,396.6 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambapo katika sekta ya madini kumekuwa na ongezeko la utoaji leseni kwa wachimbaji wadogo kutoka 290 hadi 1650 hatua inaotajwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za uchimbaji.
Sambamba na hilo, makusanyo ya maduhuli ya madini yameongezeka kutoka Sh. 105,553,514,527.16 mwaka 2021/22 hadi Sh. 193,988,549,605.59 mwaka 2025/26,Ongezeko hilo ni zaidi ya Sh. bilioni 88.4, likionyesha kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini katika mapato na shughuli za kiuchumi.

Katika sekta ya kilimo, DC Nkinda amesema Serikali imeendelea kusimamia mapinduzi ya kilimo kwa kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha na salama ambapo Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuimarisha huduma za umwagiliaji, na kwamba kuna vituo 104, vipimo vya udongo 3 na visima 96 kwa ajili ya shughuli zinazohusiana na kilimo.
Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kuwawezesha wakulima kupata mazingira bora ya uzalishaji, hususan katika maeneo yanayohitaji huduma za umwagiliaji.

Kwa upande wa mifugo, amesema Serikali imeendelea kuimarisha ufugaji kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za mifugo, ikiwemo dawa na chanjo,ambapo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa usambazaji wa dawa za ruzuku, huku jumla ya lita 1,360 za dawa na dozi 427,000 za chanjo zikitajwa kutolewa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Amesema Hatua hiyo inalenga kupunguza madhara yanayosababishwa na magonjwa ya mifugo na kuhakikisha wafugaji wanapata huduma muhimu za kinga na tiba kwa wakati.
Takwimu hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, huku Serikali ikiendelea kusisitiza matumizi ya rasilimali katika miradi inayolenga kuchochea maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.


