KAHAMA: WANAKIJIJI LOWA WAMKATAA MWENYEKITI WAKIMTUHUMU KWA UBADHIRIFU

Na William Bundala, Kahama – Shinyanga.

Wananchi wa Kijiji cha Lowa kata ya Nyandekwa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wamemkataa Mwenyekiti wa Kijiji hicho wakimtuhumu kwa makosa mbalimbali yakiwemo ubadhilifu wa fedha za Kijiji, wizi wa vifaa vya ujenzi wa shule ya sekondari ya amali Pamoja na kuuza maeneo ya Kijiji.

Wananchi hao wamemkataa Mweyekiti huyo katika mkutano uliofanyika katika Kijiji hicho, huku wakisema amekuwa na tabia ya kuwaonea wananchi na kutoa maamuzi ya uonevu na kugushi nyaraka za serikali.

“Mwenyekiti wetu amekuwa na tabia ya kuwaonea wananchi,anatoa maamuzi ya upendeleo na mbaya zaidi anawadhurumu watu viwanja kwa kugushi nyaraka sisi hatumuhitaji katika Kijiji chetu,” Wamesema wananchi hao.

Wameongeza kuwa, kuna mali za Kijiji yakiwemo matofali na mabati yaliyotolewa na aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli na kwamba hayajulikani yalipo, huku wakimtuhumu kuwaondoa makamanda wa sungusungu waliochaguliwa na Kijiji na kuweka watu wake.

“Kuna mabati bando nne tulipewa na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kahama Mh.Lembeli hatujui yalipo,lakini kuna matofali tuliazimia tujenge ofisi ya Kijiji na ofisi ya chama nayo pia hatujui yalipo na kuna faini mbalimbali wanaotozwa wananchi hatujui inenda wapi na hatupewi risiti,” wameongeza wananchi hao.

Katika hatua nyingine wananchi hao pia wamelalamikia kitendo cha Mwenyekiti huyo kuwachonganisha wananchi katika mambo ya maendeleo huku wakichukizwa na kitendo cha kuingilia majukumu ya wengine kijijini.

“Amekuwa mchonganishi anatoa maneno upande mmoja na kupeleka upande mwingine hali inayosababisha wananchi kuwa na ugomvi baina yao,lakini pia anaingilia majukumu ya viongozi wengine wa Kijiji.” Wamesisitiza wananchi hao.

Wakiongea kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nyandekwa, Malimi Ntale na Katibu wake Monica Leonard wamesema, Chama kinaungana na wananchi na kwamba hawawezi kumtetea kiongozi mbadhirifu anayetuhumiwa na Kijiji kizima.

“Sisi chama cha Mapinduzi tunaungana nanyi katika hili,haiwezekani twende na kiongozi kama huyu ambaye anatia dosari kwenye chama chetu, tupo pamoja nanyi tunawaunga mkono na uongozi wa wilaya hadi mkoa wajue kabisa wananchi hawamtaki mwenyekiti wa Kijiji chao,” walimesema Viongozi hao wa CCM, kata ya Nyandekwa.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu tarafa wa dakama Salakana James amesema kuwa tume ya uchunguzi itakwenda kuchunguza tuhuma hizo na kuwaambia wananchi kuwa mweyekiti huyo atapumzika uongozi kwa muda ili kupisha uchunguzi huo.

“Niwaombe wananchi muwe na Subira,vyombo vya uchunguzi vitakuja hapa na watafanya uchunguzi wao na kikubwa nawaomba sana mtoe ushirikiano kwa tume ya uchunguzi na wote mliotoa malalamiko yenu mjitokeze kutoa Ushahidi ili zoezi liwe rahisi,” amesisitiza James.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyandekwa, Lutahundi Katoto ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya kazi kwa juhudi zote ili kujiletea maendeleo na kwamba yuko nao bega kwa bega katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika Kijiji cha Lowa na kata ya Nyandekwa kwa ujumla.

“Niwaombe wananchi tusubiri maamumuzi ya vyombo vya uchunguzi,kikubwa sasa tujikie katika kufanya kazi ili kujiletea maendeleo katika Kijiji chetu,Mimi kama diwani wenu nipo bega kwa bega kuhakikisha tunapata maendeleo” Amesema Katoto.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Lowa, Masudi Buseli ambaye anatuhumiwa na wananchi amesema hausiki na tuhumua hizo na ameshangazwa kwa kitendo cha kutopewa nafasi ya kujitetea katika mkutano huo na kwamba hizo ni chuki za kisiasa zinazofanywa na baadhi ya viongozi wenzake waliotangulia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *