KAHAMA MWENYEJI MKUTANO MKUU WA TFF

Na William Bundala – Kahama

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) linatarajia kufanya mkutano mkuu  February 27 na 28, 2026 wilayani ya Kahama mkoani Shinyanga, ikiwa ni kwa mara ya kwanza shirikisho hilo kufanyika mkutano mkuu wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari, katika Manispaa ya Kahama mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF Azan Mufti amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo, ni heshima kubwa na wakazi wa kahama na kuwataka kuchangamkia fursa kwa uwepo wa ugeni huo mkubwa.

”Mkutano huo utatoa nafasi kwa wadau wa soka kubadilishana mawazo, kujadili changamoto na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu nchini,hivyo ni fursa kubwa kwa wana Kahama kufanya biashara mbalimbali kwa ugeni huu mkubwa tutakaokuwa nao” Amesema Mufti.

Sambamba na hayo Mufti amesema kuwa mkutano huo utajadili mambo mengi kuhusu soka letu nchini Pamoja na ujenzi wa uwanja wa kisasa Kahama ambao utaweza kuingiza watu 7,000.

“Huu ni mkutano muhimu sana kwetu,maana tutajadili mambo mengi kwa mafanikio ya soka letu ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa manispaa ya Kahama ambao utaingiza watu 7,000” Ameongeza Mufti.

Awali akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kuinua soka la ukanda wa ziwa Mufti amesema kuwa kuna malengo mengi  ambayo wamejiwekea katika kukuza soka ikiwa ni Pamoja na kujenga chuo cha michezo manispaa ya Kahama ambacho kitazalisha wachezaji mahili watakaofundishwa na walimu wenye ujuzi.

“Tunayo malengo mengi Kuhusu soka letu moja wapo ni kuhakikisha tunajenga chuo cha michezo hapa Kahama na kuanza kuwafundisha watoto wenye vipaji ambao watatoka hapa wakiwa ni wachezaji wazuri” Amesisitiza Mufti.

Kwa mujibu wa mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF Azan Mufti amesema kuwa Aidha, ameongeza kuwa Rais wa TFF Wallece Karia anatarajiwa kuwasili Kahama Febuary 25 kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kufanyika rasmi kwa mkutano huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Mpira wa miguu wilayani Kahama (KDFA) Salum Hussein ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wajumbe wote wa mkutano mkuu katika manispaa ya Kahama na kwamba siku ya tarehe 26 Rais wa TFF Wallece Karia Pamoja na wajumbe wengine watapata nafasi ya kushuhudia mechi ya mpira wa miguu katika uwanja wa manispaa ya Kahama.

“Niwakaribishe wajumbe wote wa mkutano mkuu katika manispaa ya Kahama,Kahama iko salama na ina watu wakarimu sana na tarehe 26 kutakuwa na mechi kubwa katika uwanja wetu wa manispaa ambapo wajumbe wa mkutano mkuu na Rais wetu wa TFF Wallece Karia watapata nafasi ya kushuhudia mechi hiyo,hivyo wananchi wote wanakaribishwa kuja kuangalia mchezo huo” Amesema Hussein.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *