
Na Clavery Christian – Kagera
Zaidi ya wahamiaji haramu 800 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera ndani ya mwezi Juni/Julai 2025 na tayari baadhi yao wamerudishwa katika nchi zao za asili, katika operesheni maalum ya kuondoa wahamiaji haramu mkoani humo.
Taarifa hiyo ilitolewa na Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba, ambapo amesema kuwa operesheni hiyo ni endelevu na inalenga kuhakikisha usalama wa mipaka ya Tanzania unalindwa ipasavyo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

“Kwa mwezi mmoja wa Juni tumekamata wahamiaji haramu zaidi ya 700, ambao Burundi ni 514, Uganda 59, Rwanda 41, Kenya 1, DRC 9 Ethiopia 1, Wachina 5, Pakistan 1 na watanzania 51 na watu wengi 41 waliokuwa na utata wa uraia na kukutwa na makosa ya uhamiaji haramu ambao jumla yao ni 725 kwa mwezi Juni. Alisema Afisa Uhamiji Kagera
Aidha amesema kuwa kwa mwezi wa julai tayari wilaya ya Missenyi wamewakamata wahamiaji 74 kutoka Burundi, Biharamulo 35, Ngara 26 na taratibu za kuwarejesha kwao zinaendelea huku wengine wakiwa tayari wameisha rejeshwa kwao.
Ameongeza kuwa wahamiaji hao wengi wao hutokea nchi jirani na huingia kwa njia zisizo rasmi, na wengine hukutwa wakijihusisha na shughuli zisizo halali, jambo linalohatarisha usalama wa taifa.

Amewataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahamiaji haramu wote.
“Kipindi hiki ni nyeti, taifa linaelekea kwenye uchaguzi. Hivyo, tunahitaji kila raia kushiriki kulinda amani na mipaka yetu,” alisisitiza.
Operesheni hiyo inaendelea kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha mkoa unakuwa salama na huru dhidi ya wageni wasio halali.