KAGERA YAJIPANGA KUINUA PATO LA MKOA KUPITIA UFUGAJI WA SAMAKI WA VIZIMBA

Na Clavery Christian – Kagera.

Katika kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inazidi kuleta tija kwa Wananchi na kuchangia pato la Mkoa wa Kagera, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeandaa semina maalum iliyo wahusisha Wavuvi, Wadau wa uvuvi na Maafisa Uvuvi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera, iliyolenga kutoa elimu juu ya ufugaji wa Samaki kwa njia ya vizimba Ziwa Victoria.

Akizungumza wakati wa kufungua semina hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa alisema sekta ya uvuvi imeendelea kuwa nguzo muhimu ya kiuchumi kwa mkoa huo, huku akisisitiza kuwa ni lazima kuwekeza katika mafunzo, teknolojia bora na kuhakikisha upatikanaji wa masoko, ili kuinua pato la Wananchi .

Amesema, “sekta hii ina uwezo mkubwa wa kuondoa wananchi kwenye umasikini ikiwa tutawekeza kwenye elimu, teknolojia ya kisasa na masoko ya uhakika.”

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi wa Mkoa wa Kagera, Efrazi Mukama alieleza kuwa wao kama wataalamu wa sekta hiyo wamejipanga kuwa karibu na wafugaji wa samaki ili kuwapa elimu ya kutosha juu ya matumizi ya teknolojia mpya ya vizimba.

 “Tunalenga kuhakikisha kila mfugaji anaelewa namna bora ya kufuga kwa kutumia vizimba ili kuongeza tija na kudhibiti uvuvi usio endelevu,” alisema Mukama.

Naye mmoja wa wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, George Mgasha alisema kuwa teknolojia hiyo itasaidia kupunguza uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na kuongeza uzalishaji wa samaki kwa njia endelevu.

“Vizimba vina faida nyingi, vinadhibiti uvuvi holela na vinakuza uchumi wa familia kupitia mauzo ya samaki,” alisema Mgasha.

Hata hivyo, kupitia semina hiyo, wadau wa uvuvi wameiomba serikali kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo mitaji, upatikanaji wa chakula cha samaki, na miundombinu ya usafirishaji, ili kuhakikisha bidhaa za Samaki zinafika sokoni kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *