KAGERA: WAVUVI WAPEWA DARASA USAJILI WA BIASHARA, ULIPAJI KODI

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera, imetoa elimu kuhusu mlipa kodi kwa wavuvi wanaoishi katika mwalo wa Marehe, ulioko kijiji cha Marehe, kata ya Rubafu, mkoani Kagera.

Hayo yameelezwa na Afisa Elimu na Mawasiliano wa TRA Kagera, Rwekaza Rwegoshora wakati akizungumza na wananchi katika mwalo wa Malehe kwenye zoezi la utoaji elimu kwa Wafanyabiashara wa mipakani.

Rwegoshora amesema kuwa lengo kuu ni kuwasogezea huduma karibu wananchi hao ili kupunguza shida ya kusafiri umbali mrefu  kufuata huduma za usajili wa biashara na kulipa kodi katika Manispaa ya Bukoba, yalipo makao makuu ya TRA.

Amesema zoezi la kuhamasisha jamii kuhusu kodi linaendelea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali yenye mialo mkoani Kagera, ambapo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata elimu hiyo, pamoja na kusajili biashara zao.

Aidha, Rwegoshora amebainisha kuwa kufikisha huduma hii kwa wananchi waishio katika mwalo wa Marehe kutaongeza idadi ya wafanyabiashara wapya, kwani baadhi ya wananchi walikuwa wanafanya biashara bila kufuata utaratibu wa usajili, hivyo elimu  hiyo itachangia kuongeza mapato ya serikali.

Katika hatua nyingine, amewasisitiza wananchi wa maeneo hayo kufuata taratibu za kuingiza bidhaa nchini kupitia milango ya kiforodha, kwani kutokufuata sheria hizo kunaweza kuikosesha serikali mapato muhimu ambayo ni ya msingi kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

Miongoni mwa wanufaika wa elimu hiyo akiwemo Paulo Nshekanabo Ribent, amesema kuwa elimu aliyopata imemsaidia kusajili biashara yake, ambayo awali hakuwa na uelewa wa namna ya kufanya hivyo.

Nshekanabo pia amewashauri wananchi wengine wa eneo hilo kutumia elimu waliyoipata ili kusajili biashara zao na kulipa kodi kwa wakati na kuishukuru TRA kwa kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *