KAGERA KUWA YA KISASA YENYE VIVUTIO VYA UTALII – RC MWASSA

Na Clavery Christian, Bukoba – Kagera.

Jumla ya shilingi Bilioni  9 zinatarajia kujenga  jengo la kisasa la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, lenye ukumbi wenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 350.

Hayo yamesema na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya eneo la mradi kwa Mkandarasi ambapo alisema kuwa Mkoa Kagera unakwenda kuwa miongoni mwa mikoa ya kisasa na kuwa sehemu ya kivutio kwa wageni.

Hajat Mwassa, amesema ofisi ya sasa ya mkuu wa mkoa wa Kagera  ina miaka zaidi ya sitini (60) na ubora wake umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kupitiwa na tetemeko mwaka 2016, na kwamba ziwa linaendelea kusogea  na nyumba nyingi za watumishi zimemezwa.

Hata hivyo amesema Mkandarasi ameshalipwa asilimia 25 ya fedha kati ya shilingi bilioni 4.6 za mradi wa ujenzi wa jengo hilo awamu ya kwanza.

Awali, Mhandisi Raphael Nyatega kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera ,alisema  mradi huo wa ujenzi  ulianza mwaka wa fedha 2024/2025 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha  2025/2026.

Mhandisi Nyatega alisema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu mbili na awamu ya kwanza itakuwa na ofisi kuu kwa maana ofisi ya mkuu wa Mkoa na wasaidizi wake, Katibu Tawala wa Mkoa na Wasaidizi wake, ukumbi wa mikutano utakao kuwa na uwezo wa kuwa na watu 350, mgahawa mkubwa wa kisasa, ofisi ya habari maelezo na ofisi ya uwekezaji.

Alisema usanifu wa jengo hilo umezingatia nafasi ya Mkoa kimkakati  katika uwekezaji na mradi huo wa ujenzi Awamu ya kwanza umesainiwa mkataba wa shilingi bilioni 4.6 na utakamilika kwa muda wa miezi 12, na awamu ya pili itakuwa ujenzi wa jengo la watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, itakayokuwa na ofisi za wakuu wa vitengo pamoja na maofisa wote na wasaidizi wa ofisi.

Alisema awamu ya pili bado ipo katika hatua za usanifu inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 4.4 na mpaka kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa  ofisi ya mkuu wa Mkoa  wa Kagera  unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.

Naye mshauri mwelekezi katika  mradi huo  mbunifu majengo  ( Architect )Gozbert  Kakiziba kutoka kampuni ya ( GOZTECTURE GROUP LTD) amesema jengo litakuwa imara halitapata shida ya kupitiwa na tetemeko na litakaa zaidi ya miaka mia moja.

Mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo ni   Haamid Ashraf kutoka kampuni ya  ( Skywords Construction Co.ltd )

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *