KADOGOSA AONGOZA IBADA YA KUMUOMBEA RAIS SAMIA NA TAIFA MKOANI SIMIYU..

Na Saada Almasi -Simiyu

Katika kuendelea kulikabidhisha Taifa mikononi mwa Mungu kwa dua na maombi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli Tanzania Masanja Kungu Kadogosa amefanikisha dua maalum ya kumuombea Rais Samia pamoja na marehemu baba yake iliyohusisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo pamoja na viongozi wa dini na serikali.

Akiwa kijijini kwao Mwakibuga wilayani Bariadi mkoani Simiyu ambapo dua hiyo imefanyika, Kadogosa amewaomba wananchi wa Simiyu kuifurahia amani waliyo nayo kwani ikitoweka ni vigumu kuirudisha huku akiwataka kuendelea kuiombea nchi na kumwombea Rais wa nchi kutokana na miradi anayoitekeleza kwa faida ya wananchi

“Mimi ni mwakilishi wa Serikali nasimamia reli ninaona jitihada anazozifanya Rais wetu ule mradi wa reli umechukua pesa nyingi sana si kwa ajili ya Rais ni kwa matumizi ya kila mmoja hapa hivyo tumuombee na tuifurahie hii amani kwani ikitoweka hatuipati kirahisi” mkurugenzi Kadogosa

Aidha ameongeza kuwa hakuna jambo jema kama kukutanika pamoja kwa nia moja kutokana na kwamba hakuna anayejua ni maombi ya nani yatapokelewa

“kusanyiko hili litawafanya wengine wamjue Mungu na hatujui ni maombi ya nani yatapokelewa lakini hili ni jambo jema” – Kadogosa

Sambamba na hilo mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga akimuwakilisha mkuu wa mkoa huo Kenani Kihongosi amesema kuwa hakuna mahali ambapo kuna maendeleo pasi na kuwa na amani na huku akiutaja mradi wa bilioni 400 wa maji ya ziwa Victoria hapa Simiyu kama sehemu ya maendeleo ambayo yanawapasa wananchi kuendelea kumuombea raisi pamoja na amani ili maendeleo yazidi kupatikana

“Hakuna maendeleo bila amani huyu Raisi tunayemuombea leo analeta maji ya ziwa Victoria ili wewe mwananchi uwe na chaguo maji ya visima virefu,maji ya mvua au maji ya ziwa victoria kwa nini tusimuombee mama kwa msaendeleo haya” – Simalenga

Kwa upande wake aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu Yahya Nawanda amewashukuru Wananchi wa mkoa huo kwa kujumuika nae katika maombi pale alipokuwa anapitia kipindi kigumu huku akiwataka kuishi na watu vizuri kwani kesho yao hawaijui.

“Niseme tu kuwa nawashukuru sana kwa kuwa nami katika kipindi kigumu nilichopitia najua mliniombea sana na Mungu ametenda na niwaombe endeleeni kuishi na watu vizuri kwani kesho ya kila mmoja ni Mungu pekee ndiye anayeijua” – Yahya Nawanda

Nae Sheikh mkuu wa simiyu Issa Kwezi amesema kuwa dini ni sawa na njia ama nyumba ambayo tunakula pamoja lakini kila mmoja analala chumba chake hivyo tuishi kwa kuheshimiana na kutengeneza mahusiano mazuri na watu 

“Nimeona umati wa watu hapa na wote wamekuja kwa sababu yako laiti ungekuwa na mahusiano mabaya ama huwaheshimu wasingepokea wito wa dua hii,hili ni funzo tupendane tuheshimiane kwa maslahi mapana ya nchi”Sheikh Kwezi

 Akihitimisha ibada hiyo padri Albert Izengo wa parokia ya Malili aliyeongoza ibada hiyo amesema kuwa amani ya Tanzania ni tunu sote tuilinde bila kujali itikadi za chama wala dini kwani sisi sote ni wamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *