
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) imesema imekamilisha uchunguzi uliokuwa unafanywa ili kuona kama kuna ukiukwaji wa sheria za uwindaji baada ya kuonekana kwa video ya Mwindaji wa Marekani Josh Bowmer akifurahia kuwinda mamba mkubwa nchini Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo January 02,2024 na kitengo cha uhusiano kwa uma -TAWA imesema kuwa Kwa mujibu wa taratibu za mkataba wa kimataifa wa CITES, Tanzania imeruhusiwa kuwinda mamba wasiozidi 1,600 kwa mwaka ambapo mpaka sasa mamba 39 tu kati ya 1,600 wamewindwa kutoka kwenye mgawo wa Taifa wa mwaka 2023.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamba anayeonekana kwenye picha jongefu (video clip) iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, aliwindwa katika kitalu cha Lake Rukwa GR kwa kibali halali namba MP-0001792 kilichoanza tarehe 12/08/2023 hadi 09/09/2023”.
TAWA imewahakikishia Wananchi kuwa uwindaji wa wanyamapori nchini unazingatia Sheria na taratibu za ndani ya Nchi na zile za kimataifa na Mamlaka inawatoa hofu kuwa taratibu hizi zinasimamiwa ipasavyo na pale panapotokea ukiukwaii hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa sheria.


